MHE. MTANDA AWATAKA ASKARI WALIOFANYA VIZURI 2024 KUWA CHACHU KWA WENGINE 2025
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewapongeza Wakaguzi na Askari wote wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza waliotekeleza vizuri zaidi kwenye majukumu yao katika maeneo yao ya kazi hivyo kupelekea kupata vyeti vya Sifa na zawadi kwa mwaka 2024.
Mhe. Mtanda ametoa pongezi hizo leo Februari 08, 2025 alipokuwa akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Familia ya Polisi 2025 yaliyoadhimishwa katika viwanja vya FFU Mabatini, Jijini Mwanza na kuwataka Maafisa na Askari waliofanya vizuri kuwa chachu kwa wengine ambao hawakufanya vizuri.
Aidha RC Mtanda amewapongeza na kuwasihi kuendelea na ari na moyo huo wa kuchapa kazi kwa bidii, uaminifu, nidhamu na maarifa ya kupigiwa mfano, ujasiri, kujituma, kupenda kazi, kuwa na kauli nzuri na kutoa huduma nzuri inayozingatia haki kwa wananchi.
Kadhalika Mhe. Mtanda amesema Vyeti vya Sifa na zawadi zilizotolewa leo siku ya Familia ya Polisi ni kumbukumbu kwa sisi tuliopo na wanaokuja kwamba hawa Wakaguzi na Askari ni miongoni mwa Askari waliolifanyia vizuri zaidi katika jeshi la polisi na Wananchi kwa ujumla kwa mwaka 2024/2025.
“Ni matumaini yangu kuwa mafanikio yao yatakuwa kichocheo kwa Askari wengine ambao hawakupata vyeti vya Sifa na zawadi leo kuongeza bidii zaidi ili waweze kufikia na hata kuzidi viwango vya ubora wa kufanya kazi vizuri zaidi”.
Mhe. Mtanda pia amesema tunajivunia mchango mkubwa unaotolewa na Jeshi la Polisi katika kulinda usalama pamoja na maisha na mali za raia. Amesema anatambua kazi kubwa na nzuri waifanyayo iliyotufikisha hapa tulipo sasa.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP Wilbrodi Mtafungwa amesema maadhimisho ya Siku ya Familia ya Polisi ni kiashiria cha kuwa mwaka mpya wa Kipolisi umefunguliwa rasmi amabapo wanashiriki pamoja kama familia kuadhimisha sherehe hiyo.
DCP Mtafungwa ameendelea kwa kusema kuwa zawadi zilizotolewa ni namna ya kutambua mchango na kazi nzuri iliyofanywa na Askari pamoja na Maafisa hao katika kutekeleza majuku ya jeshi la polisi la kulinda usalama wa raia na mali zao.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.