MITAMBO YA KUOPOA MAGUGUMAJI KUWASILI MWISHONI MWA MWEZI JULAI
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita imekamilisha mchakato wa manunuzi ya mitambo miwili maalum ya kuopoa magugumaji aina ya Salvinia na Mtambo mkubwa wa kuondoa magugu maji aina ya Lutenda kabla ya Mwisho wa Mwezi Julai 2025.
Mhe. Waziri Mkuu ametoa tamko hilo mapema leo alipokuwa akikagua maendeleo ya udhibiti wa gugumaji aina ya Salvinia eneo la Kigongo na Busisi (Ziwa Victoria) ambapo amewashukuru wananchi na kwa jitihada za awali za kutumia mitumbwi kusafisha ziwa.
Waziri Mkuu amesema Serikali ina mpango wa kusafisha maeneo yote yanayozunguka ziwa victoria ikiwemo mikoa yote ya Kanda ya Ziwa ili kuhakikisha gugumaji hilo linaondolewa na hali hiyo haitokei tena.
Akisoma taarifa ya magugumaji hayo kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mwenyekiti wa timu ya kuondoa Magugu Maji Ziwa Victoria Dkt. Kaniziro Manyika amesema magugumaji hayo yameathiri mifumo ya ikolojia, shughuli za usafiri na usafirishaji na shughuli za uvuvi katika ziwa Victoria.
“Kwa kipindi cha Mwezi Februari hadi kufikia tarehe 18 Mei 2025 kiasi cha tani 840 kimeopolewa, zoezi hili limesaidia kuondoa changamoto ya usafiri na usafirishaji katika eneo la Kigongo-Busisi.”. Amebainisha.
Awali, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema Katika kushughulikia changamoto hiyo kwa kipindi cha muda mfupi jumla ya tani 840 za gugumaji jipya aina ya Salvinia molesta limeopolewa na kufungua njia ya usafiri na shughuli za kiuchumi katika eneo la Kigongo-Busisi.
Mhandisi Luhemeja ameendelea kwa kusema kwa sasa eneo hilo halina changamoto tena ya Gugumaji ya aina hii mpya na juhudi zinaendelea katika eneo hilo la Kigongo-Busisi za kushughulikia Gugumaji la Asili aina ya Lutende. Jumla ya Ekari 65 zimeshughulikiwa katika kipindi cha wiki moja na lengo ni kumaliza Ekari zote kabla ya tarehe 10 ya Mwezi Juni-2025.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.