Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. David Silinde amesema mradi wa umwagiliaji wa Ibanda–Igaka unaotekelezwa katika Mikoa ya Geita na Mwanza utaendelea kutekelezwa kama ulivyopangwa licha ya kuwepo kwa changamoto ya madai ya fidia kutoka kwa baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Sengerema, Mkoa wa Mwanza.

Mhe. Silinde ametoa kauli hiyo Januari 10, 2025 wakati wa kikao kifupi na Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw. Balandya Elikana aliyewasilisha taarifa ya sintofahamu iliyojitokeza kuhusu fidia kwa wananchi wanaotakiwa kupisha maeneo yao kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Naibu Waziri amesema Wizara ya Kilimo haina fungu la moja kwa moja la kulipa fidia lakini serikali itaendelea kutumia njia ya elimu, mazungumzo na uhamasishaji kwa wananchi ili waelewe umuhimu wa mradi huo katika kuongeza uzalishaji wa kilimo, usalama wa chakula na ajira.

“Mradi hautasimama. Tutatumia elimu na njia nyingine za mazungumzo ili kuhakikisha utekelezaji unaendelea,” amesema Mhe. Silinde.

Akizungumza katika kikao hicho Bw. Balandya alisema sekta ya kilimo ni miongoni mwa sekta muhimu zinazochangia uchumi na kuajiri watu wengi, hivyo kuna umuhimu wa kuhakikisha kilimo kinafanyika kwa tija kupitia umwagiliaji.

Amesema Mkoa wa Mwanza umebarikiwa kuzungukwa na Ziwa Victoria jambo linalotoa fursa kubwa ya kuendeleza kilimo cha umwagiliaji badala ya kutegemea mvua, sambamba na kusaidia kupunguza tatizo la ajira kwa vijana.

“Tuna vijana wengi hapa Mwanza wasio na ajira. Tunategemea kilimo hususani cha umwagiliaji kiwe suluhisho la changamoto hiyo”.

Bw. Elikana amezihimiza Halmashauri kuweka mazingira wezeshi kwa shughuli za kilimo na mifugo kwa kutumia fedha za maendeleo kujenga miundombinu muhimu kama maeneo ya umwagiliaji, majosho ya mifugo na kutenga maeneo maalum kwa vijana kujihusisha na kilimo na ufugaji.

Ameeleza kuwa ingawa matumizi ya fedha za maendeleo kwa sasa yana masharti, bado kuna fursa ya kuzitumia kujenga miundombinu itakayochochea ajira na maendeleo kwa vijana.

Mradi wa Ibanda–Igaka, unaogharimu takribani Shilingi bilioni 35, upo mpakani mwa Wilaya ya Sengerema (Mwanza) na Mkoa wa Geita.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.