Halmashauri ya Wilaya Sengerema imepokea Tshs. Bilioni 2.16 katika mwaka wa fedha 2025/26 kwa ajili ya kujenga miradi 9 ya elimu zikiwemo shule mpya 4 fedha zilizokusudiwa kupunguza msongamano darasani na kuwapunguzia wanafunzi umbali wa kufuata elimu.

Akikagua miradi ya Elimu leo tarehe 20 Januari 2026 wilayani humo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewataka viongozi na watendaji wa halmashauri hiyo kuhamasisha wazazi na walezi wanawapeleka watoto shule katika ngazi zote kuanzia awali, msingi na kidato cha kwanza.

Mhe. Mtanda amewataka watendaji kuhakikisha wanapita nyumba kwa nyumba kuzungumza na wazazi na ili wawapeleke watoto shuleni huku akitolea mfano wa wanafunzi wa kidato cha kwanza kuwa ni asilimia 19 pekee (1561) ya walioandikishwa (7987) ndio wameripoti mpaka sasa.

Ameongeza kuwa wazazi wahamasishwe kuchangia mpango wa chakula shuleni ili wanafunzi wawe na nguvu ya kusoma na kupokea wanachofundishwa kwani wana uhakika wa chakula kilichozingatia lishe bora wakati wa masomo.

“Chakula kwa wanafunzi ni wajibu wa wazazi, hatuwezi kuwa na maendeleo mazuri kitaaluma ikiwa watoto wanashinda njaa shuleni hivyo twendeni tukahamasishe wazazi watoe michango halali iliyoidhinishwa na mamlaka.” Amesema Mhe. Mtanda

Akizungumza katika nyakati tofauti wakati akakikagua ujenzi wa shule mpya za Msingi Sima na Tabasamu Mhe. Mtanda ameagiza kasi ili kufanya ukamilishwaji wa haraka wa miradi yote hadi kufikia februari 28, 2026 ili wanafunzi wapate elimu katika miundombinu kamili.

Aidha, amewataka Wakala ya Maji vijijini (RUWASA) kuhakikisha wanapeleka huduma ya maji kwenye Taasisi na kwa wananchi wa Kata ya Sima kwani tayari serikali imejenga mradi mkubwa wa maji na kwa TARURA amewataka kurekebisha barabara ya kwenda kwenye shule mpya ya Tabasamu.

Akizungumza na wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha sita katika shule ya sekondari Mtunduru Mhe. Mtanda amewataka kusoma kwa bidii na kuacha kujihusisha na mapenzi wawapo shuleni na wazazi kuhakikisha wanawapa nafasi watoto wa kike kupata elimu kama wanavyopata wa kiume.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.