Wataalamu kutoka Mkoa wa Mwanza wakiongozwa na Afisa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa huo Bi. Janeth Shishila wapo Mkoani Morogoro katika Mafunzo ya siku mbili ya Mradi wa Advancing Gender Equality in Tanzania (PAMOJA) unaolenga kukuza Usawa wa Kijinsia nchini.

Mradi huo unaotekelezwa kwa kushirikiana kati ya Ofisi ya Rais -TAMISEMI na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wizara ya Fedha pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mkopo wenye masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia utadumu kwa kipindi cha mwaka 2024/25 hadi 2028/29.

Mafunzo haya yatafanyika kwa siku mbili yaani leo tarehe 13-14 Novemba 2025 katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Jordan ukiikutanisha mikoa ya Arusha, Geita, Kagera, Mara, Mwanza, Rukwa, Shinyanga, Simiyu, Singida na Tabora na halmashauri 40.

Mratibu wa Mradi wa PAMOJA kutoka Wizara ya Maendeleo Ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Bi. Adventina Kato ametoa rai kwa wataalamu hao kutekeleza mradi kwa kufuata miongozo ya mradi ili kujihakikishia kufikia malengo ya kimkataba baina ya serikali na wahisani ambao ni benki ya Dunia.

Mradi huo unatekelezwa kuanzia Julai (Hatua za awali) 2025 kwa miaka mitano kwa thamani ya Dola Milioni 100 ambapo asilimia 87 ni kwa ajili ya Bara na 13 ni za upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kwamba pamoja na mambo mengine fedha hizo zimeelekezwa zaidi kwenye uwezeshaji wanawake kiuchumi.

Aidha, amebainisha kuwa kwa siku za mbeleni mradi huo unaotarajiwa kuzinduliwa rasmi mwanzoni mwa mwezi Disemba mwaka huu halmashauri tano zinatarajiwa kuongezwa ikiwemo halmashauri ya wilaya ya Ukerewe kutoka mkoani Mwanza ambayo kwa sasa haijajumuishwa.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.