Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe Mhandisi Robert Gabriel leo tarehe 12 Julai, 2022 amepokea Mwenge wa Uhuru katika kijiji cha Mwamhembo-Malya wilayani Kwimba ukitokea Mkoani Simiyu ambapo amesema utakimbizwa kwenye jumla ya KM 563 eneo la Nchi kavu na 'Nautical Miles' 86.3 eneo la Maji ziwa Victoria.
Aidha, amemshukuru Mhe Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya Maendeleo Mkoani humo katika Sekta za Elimu, Afya, Miundombinu na Maji na amebainisha kuwa Mwenge wa Uhuru utaifikia Miradi 52 yenye thamani ya zaidi ya Tshs. Bilioni 18.7 kati ya hiyo 15 itawekewa mawe ya msingi, 29 itazinduliwa, 3 itafunguliwa na 5 itakaguliwa.
"Mwenge wa Uhuru utafanya ukaguzi kwenye miradi ya anuani za makazi inatotekelezwa katika Halmashauri zote ambapo hadi kufikia tarehe 7. 3. 2022 jumla ya nyumba 653,827 zimewekewa namba sawa na asilimia 118.54 hivyo kuvuka lengo lililowekwa. Jumla ya Anuani zilizosajiliwa katika mfumo ni 670,407 ambapo utekelezaji wa Mkoa umekamilika kwa asilimia 102." Amefafanua.
Vilevile, amesema zoezi la uwekaji Nguzo zinazoonesha majina ya Barabara limekua likiendelea vema Mkoani humo na kufikia tarehe 30 Juni, 2022 jumla ya Nguzo zilizotengenezwa ni 31,525 na kufanya Utekelezaji kukamilika kwa asilimia 104.7
Mhe. Mhandisi Gabriel amesema Mkoa huo umeendelea kutekeleza Kaulimbiu ya Mapambano dhidi ya Lishe duni, Mapambano dhidi ya Ugonjwa wa UKIMWI/VVU, na amebainisha kuwa yameendelea kupungua kutoka asilimia 15.1 hadi asimilia 8.1 mwaka hadi mwaka na kwamba vijana wameendelea kuwezeshwa kiuchumi kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, Ndugu Sahil Nyanzabala ameziagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha fedha wanazokopeshwa Vijana zinarejeshwa kwa wakati ili ziweze kukopeshwa tena kwa vikundi vingine na kuwasaidia kujikwamua kwenye shughuli mbalimbali kama za Kilimo, ujasiriamali, uvuvi, biashara na ufugaji.
Katika wakati mwingine, Mhe. Mkuu wa Mkoa amemkabidhi Mwenge wa Uhuru Mhe. Johari Samizi, Mkuu wa Wilaya ya Kwimba utakaokimbizwa leo wilayani humo chini ya Kaulimbiu ya Kitaifa 2022 'Sensa ni Msingi wa Mpango wa Maendeleo, Shiriki kuhesabiwa tuyafikie Malengo ya Taifa'..
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.