Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Bw. Ismail Ali Ussi ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa kwa utekelezaji wa viwango wa miradi na dhamira ya dhati ya kusogeza huduma za kijamii kwa wananchi.
Ametoa pongezi hizo mapema leo Agosti 31 katika nyakati tofauti akiwa katika Kata ya Bukokwa wakati akiongea na mamia ya wananchi waliojitokeza kuulaki mwenge wa uhuru ulipofika kukagua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi ya Kituo cha Afya na Maduka.
Akiweka jiwe la Msingi katika Kituo cha Afya Bukokwa ndugu Ussi amesema Viongozi wa Halmashauri hiyo wameonesha uzalendo kwa kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto tena kwa kuweka mfumo wa kutoa huduma bila malipo ili kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano.
Akiongea katika soko la Bukokwa kwenye uwekaji wa jiwe la msingi kwa maduka 20 ya awamu ya kwanza kati ya 60 Bwana Ussi amewasifu kwa kubuni mradi huo unaogharimu Tshs. Milioni 160 lakini kwa malengo ya kimkakati ya kuhakikisha wanakusanya milioni 36 kwa mwaka kupitia kodi ya pango la vibanda.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Bw. Benson Mihayo amebainisha kuwa Buchosa imejipambanua katika kuhakikisha wanainua uchumi wa wananchi wao kwa kuwasogezea huduma za kijamii ili wafanye uvuvi na kilimo kwa tija.
Mwenge wa uhuru umekagua shughuli za mapambano dhidi ya Malaria katika Zahanati ya Bukokwa ambapo Halmashauri hiyo inatekeleza afua za kupambana na malaria kama kutoa elimu kwa jamii juu ya athari na namna bora ya kujikinga na malaria na kuzingatia matumizi sahihi ya dawa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.