Mkoa wa Mwanza umempokea Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya aliyewasili leo Februari 14, 2026 kwa ziara maalum ya Kikazi inayolenga kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi.

Mara baada ya kuwasili, Mhe. Mmuya amepokelewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Balandya Elikana katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.

Ziara hiyo inalenga kushiriki Kliniki ya Maombi ya Hati za Ardhi pamoja na kusimamia masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya ardhi.

Akiwa mkoani humo, Mhe. Mmuya atashiriki zoezi maalum la utoaji wa hati miliki, utatuzi wa migogoro ya ardhi na utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu taratibu na umuhimu wa umiliki halali wa ardhi.

Kliniki hiyo inatarajiwa kufanyika katika Ofisi ya Kata ya Igoma, jijini Mwanza, ambapo wananchi watapata fursa ya kuwasilisha maombi, kupata ushauri wa kitaalamu na kutatuliwa changamoto zao za ardhi papo kwa papo.

Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuboresha huduma za sekta ya ardhi na kuhakikisha migogoro inapungua huku umiliki wa ardhi ukiimarishwa kwa manufaa ya wananchi na maendeleo ya Mkoa wa Mwanza.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.