NIA YA SERIKALI KILA MWANANCHI AUNGANISHIWE MAJI NYUMBANI KWAKE - WAZIRI MKUU
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.) amesema dhamira ya Serikali ya awamu ya Sita ni kuhakikisha wanasogeza huduma ya maji katika makazi ya wananchi ili mama asibebe tena ndoo kichwani bali mkononi na kuingiza ndani.
Mhe. Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Mei 18, 2025 alipokuwa akiwasalimia wananchi wa Hungumalwa Wilayani Kwimba mara baada ya kuzindua mradi mkubwa wa maji na kuwahakikishia wanachi hao uhakika wa kupatikana kwa kipindi chote maji hayo yaliyounganishwa kutoka ziwa victoria.
Aidha, Mhe. Majaliwa amesema Serikali inaendelea kuangalia gharama za uendeshaji na matumizi kupitia jumuiya za watumia maji ili kila mwananchi anaetumia maji alipe gharama za maji kulingana na kiasi anachotumia na kwa gharama nafuu.
“Lengo la Serikali yenu ni kupatikana kwa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa Hungumalwa kwa 100%”.
Awali, akisoma Taarifa ya mradi huo Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Mwanza Mhandisi Godfrey Sanga amesema Mradi huo umetekelezwa na Mkandarasi Emirate Builders Company Ltd na kusimamiwa na wataalam wa RUWASA ambapo gharama ya mkataba ni Sh. 11,004,143,176.82 na ulianza kutekelezwa mwezi machi 03, 2022 na kukamilika agosti 15, 2024.
“Mpaka sasa kazi zote zimekamilika zenye thamani ya Sh. 10,803,026,273.14 na kubaki na salio katika mkataba la Sh. 201,116,903.68”. Mhandisi Sanga.
Mradi huo wa Hungumalwa unahudumia jumla ya wakazi 24,349 wa vijiji vya Hungumalwa, Buyogo, Ilula na Kibitilwa ambapo umeongeza asilimia ya upatikanaji Maji katika wilaya ya Kwimba kutoka asilimia 77.3 kufikia 79.4.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.