Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais -TAMISEMI (Afya) Prof. Tumaini Nagu amewataka watumishi wa afya mkoani Mwanza kutumia mifumo iliyosimikwa katika vituo vya afya kwa lengo la kuboresha na kutoa huduma bora katika Jamii.
Amesema hayo leo julai 5, 2025 katika ukumbi wa Mkuu wa mkoa Mwanza alipokuwa akifanya tathimini ya Ziara yake ya siku mbili aliyoifanya mkoani humo huku akiwataka watumishi hao kuboresha huduma kwa wananchi.
“Niwapongeze kwa kazi kusimamia miradi vizuri na kusimika mifumo katika vituo vyenu kwa asilimia 99, lakini hakikisheni inatumika ili isaidie kuonesha huduma zetu,” amesema Prof. Nagu.
Vile vile, ametumia wasaa huo kuwataka watumishi wa afya mkoani humo kukusanya mapato ya ndani kutokana na huduma wanazotoa katika jamii pia amewaasa kutumia mifumo vizuri kwa lengo la kuepuka changamoto mbalimbali.
Hata hivyo, Prof. Nagu amewaomba watumishi wa afya kutumia lugha za staha kwa wagonjwa na kuzingatia maadili, muongozo na busara hasa pale wanapokuwa wanahudumia wagonjwa katika vituo vyao vya huduma kwa wananchi.
Naye, Mganga mkuu wa Mkoa Mwanza Dkt. Jesca Lebba ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuchagiza maendeleo katika Mkoa wa Mwanza hasa katika upatikanaji wa vifaa tiba, Magari ya uhakika ya kusambaza chanjo, ongezeko la wahudumu na hata uboreshaji wa makazi ya wafanyakazi wa Idara hiyo.
Kadhalika, amewapongeza watumishi wa idara ya afya Mkoa wa Mwanza kwa Utendaji kazi wao uliotukuka katika kipindi chote pasipo kukata tamaa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.