RAIS SAMIA AWATAKA WANANCHI WA MKOA WA MWANZA KUTANGULIZA UZALENDO NA KUILINDA MIRADI
*Amtaka Mtendaji Mkuu TANROADS kulisimamia kikamilifu liwe na ubora*
*Awahakikishia wananchi kasi ya kuwaletea Maendeleo*
*Ashukuru kwa mapokezi makubwa tangu amewasili Mwanza*
*Aahidi kukuza uchumi Watanzania kwa kupitia miradi *
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi wa Mkoa wa Mwanza kutanguliza uzalendo katika mradi ya maendeleo na kuepukana na aina yoyote ya wizi ambao utarudisha nyuma kasi ya umaliziaji wake.
Akizungumza leo na wananchi Wilayani Misungwi mara baada ya kupata taarifa ya mradi wa Daraja la Kigongo- Busisi, Dkt.Samia amesema huo unakuja kukuza uchumi wa Taifa na wananchi wa eneo hilo hivyo wana kila sababu ya kuulinda kwa faida yao.
"Ndugu zangu wananchi nimepita kidogo hapa kuona maendeleo ya mradi huu ambao sasa umefikia zaidi ya asilimia 70 kabla ya kukamilika,nimefarijika ila nimesikia kuna ka-mkono wa udokozi wa vifaa,kemeeni hilo na wacheni," amesisitiza Mhe.Rais.
Aidha, amemtaka Mtendaji Mkuu wa wakala wa barabara TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta kuhakikisha Daraja hilo linakuwa na ubora kwa kusimamia kila hatua na vipimo vyote vifanywe kwenye maabara za Serikali na siyo kufanywa na Mkandarasi pekee.
"Mhe.Rais Daraja hili linalojulikana kama JP Magufuli lenye urefu wa kilomita 3 limegharimu Shs bilioni 716.33 na hadi sasa Mkandarasi CCECC Construction kutoka China amelipwa Shs bilioni 368.67 na tumefikia asilimia 75 ya utekelezaji na itapitiwa na barabara kuu ya Usagara-Sengerema hadi Geita," Mhandisi Besta
Mtendaji huyo Mkuu wa wakala wa barabara nchini amebainisha mradi huo wa Daraja pia umekuwa ni darasa kwa wahandisi wa hapa nchini kutokana na kuwekwa katika kila eneo kwa lengo la kuongezewa ujuzi.
"Mhe.Dkt.Samia kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Misungwi tunaendelea kukushukuru kwa kuonesha kwa vitendo kasi ya maendeleo,miradi mingi imefanyika Jimboni kwangu kuanzia Sekta ya afya na elimu,na wananchi wa Misungwi wamefurahi sana kutujengea barabara ya Mwanangwa hadi Misasi kwa kiwango cha lami",Mhe.Alexander Mnyeti,Mbunge wa Misungwi
Akikagua Ujenzi wa Meli ya MV Mwanza inayojengwa kwa Bilioni 109 kwenye Bandari ya Mwanza Kusini Mhe. Rais amewataka watanzania kufanya kazi kwa bidii ili ukamilifu wa Meli hiyo inayotarajia kubeba zaidi ya Watu 1200 na Tani 400 za Mizigo kwa wakati mmoja usaidie kufungua uchumi wa nchi kwa kubeba mizigo.
"Tunakwenda kuwafungua watanzania kiuchumi, tunajenga Meli, Bandari na Reli viende sambasamba na sisi kufanya kazi kwa bidii ili kila kinachozalishwa kwenye mashamba yetu kiende sokoni na kazi hii inafanywa kwenye kila kona ya nchi hii," Amesisitiza Rais Samia.
Naye, Mkurugenzi wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) Erick Hamissi amesema meli hiyo imeshajengwa kwa zaidi ya asilimia 80 na kwamba mkandarasi ameshalipwa fedha hadi hatua hiyo na inatarajiwa kukamilika Mwezi Agosti 2023 na watanzania zaidi ya 200 wameajiriwa hapo wakiongozwa na wataalamu Wakorea 13 tu.
Katika wakati mwingine, Mhe. Rais amewapongeza NSSF kwa Mradi mzuri wa Hoteli ya Kisasa ambayo italeta Tija mkoani humo na akawataka kupanua huduma hiyo kwenye majiji mengine Nchini.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.