RAS BALANDYA AWAKARIBISHA VIONGOZI WA PPRA MWANZA
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw. Balandya Elikana leo Juni 18, 2024 amewapokea na kufanya nao mazungumzo Mkoani Mwanza Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti kutoka Mamlaka ya Udhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) ambao wako Mkoani humo kwa ziara ya kikazi ya kukagua na kutembelea miradi ya kimkakati inayotekelezwa.
Balandya amesema kama Viongozi wa Mkoa wanatambua mchango mkubwa unaofanywa na PPRA katika nchi kwa kuzingatia kuwa takribani 80% ya bajeti ya Serikali ni ununuzi wa umma.
Aidha ameipongeza Bodi na Menejimenti hiyo kwa usimamizi mzuri wa mfumo wa usimamizi wa Ununuzi wa Umma Kielektroniki (Nest), kwani umesaidia na kuongeza uwazi pamoja na uwajibikaji.
"Shughuli zote za manunuzi ya umma zinafanyika kupitia mfumo huu wa Nest, nina imani tukiendelea kuutumia italeta mapinduzi makubwa katika sekta nzima ya manunuzi ya umma".
Kadhalika Mtendaji huyo wa Mkoa ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia kwa kuendeleza miradi yote mikubwa ya kimkakati katika Mkoa wa Mwanza, pia ameishukuru PPRA kwa kukubali kufanya na kuidhinisha manunuzi katika miradi yote hiyo ikiwemo mradi wa daraja la Kigongo-Busisi, Soko la Kisasa lililopo mjini kati, ujenzi wa Meli ya MV. Mwanza Hapa Kazi Tu, na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mwanza
Naye Mkurugenzi Mkuu wa PPRA Bw. Eliakim Maswi amesema kwa sasa wana sheria mpya wanayoitumia ambapo Serikali imeamua kuwapa kipaumbele makampuni ya ndani katika kusimamia na kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati na maendeleo ikiwa na adhma ya kuhakikisha kuwa inayalea makampuni ya ndani.
"Kwa sheria yetu hii mpya, sasa siyo kila miradi mikubwa wapewe watu au makampuni kutoka nje, tunataka pia makampuni ya ndani yakue, mabadiliko makubwa yamefanyika chini ya Rais wetu Dkt. Samia na yataleta tija katika kuyakuza makampuni yetu ya ndani". Amesema Maswi.
Wakati huo huo Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Bw.Balandya Elikana mapema leo Ofisini kwake amefanya mazungumzo na Makamanda kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ambao wapo Mkoani humo kwa maandalizi ya sherehe za uvulishwaji nishani kwa Maofisa wake na askari siku ya kesho
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.