Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Ndg. Henry Mwaijega ametoa rai kwa Halmashauri kuhakikisha wanatumia fedha za lishe kwa ajili ya kuwahudumia watoto wa shule na makundi yaliyoainishwa kwenye muongozo ili kuleta maana ya mkataba wa lishe.

Ametoa rai hiyo leo tarehe 05 Novemba, 2025 kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wakati wa kikao cha Utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kwa Mwezi Julai hadi Septemba 2025 kilichowakutanisha wataalamu pamoja na makundi ya kijamii kama viongozi wa dini.

Ndugu Mwaijega amesema tatizo la udumavu na utapiamlo, ukondefu au uzito mdogo pamoja na udumavu wanahitaji nguvu ya pamoja kuwaokoa kutoka kwenye makundi hayo kwa kushirikiana jamii na halmashauri kwa kuhakikisha wanawafikia kwa kuwapatia lishe bora.

Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Jesca Lebba amesema kikao hicho ni cha afya kinga chenye lengo la kukumbusha watumishi na jamii kuepukana na tabia bwete inayopelekea kupata magonjwa yasiyoambukiza pamoja na kupitia utekelezaji wa afua za lishe kwa mujibu wa sheria kwa kila robo kwa ngazi ya mkoa.

Akitoa utekelezaji wa mkataba wa lishe katika kipindi cha robo ya Julai - Septemba 2025, Afisa Lishe Mkoa Bi. Sophia Lugome amesema mkoa huo una udumavu kwa 28% kwa watoto huku Magu na Buchosa wakiongoza hivyo wakurugenzi watendaji wanapaswa kuongeza nguvu katika kuibua na kushughulikia.

Aidha, ametoa wito kwa wataalamu pamoja na viongozi wa dini kushirikiana na ofisi yake kwenda kutoa elimu na kufanya uhamasishaji kwenye redio watapohitajika na amezitaja redio Jembe, Free na Afya kuwa wanashirikia nao sana kwenye utoaji elimu.

Kikao hicho kimeondoka na azimio la kuitaka halmashauri ya Kwimba ambayo ina hali duni kwenye kiashiria cha upangaji wa bajeti na kiasi kinachotolewa kwa ajili afua za lishe kuandikiwa barua ya kuwataka waeleze ni kwa nini wamewasilisha kwa asilimia 4 pekee ili waweze kusaidiwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.