Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw. Balandya Elikana amewataka wahitimu wa vyuo kutumia ubunifu, ujuzi na mafunzo waliyoyapata kujitengenezea fursa kwa kutumia rasilimali zilizopo ili kujiletea maendeleo.

Amesema hayo leo novemba 28, 2025 kwenye hafla ya kuwapongeza wahitimu (1035) katika ngazi za Astashahada, Stashahada na Shahada wa Chuo Cha Uhasibu Tanzania (TIA) kampasi ya Mwanza iliyopo katika kijiji cha Nyang’homango wilayani Misungwi ambapo alikua mgeni rasmi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa.

Bw. Balandya amelitaja ziwa Vicroria lenye rasilimali lukuki, migodi na vivutio vya Utalii kama hifadhi ya Saanane kuwa ni miongoni mwa rasilimali zinazohitaji ubunifu ili kujenga fursa kubwa ya kujiendeleza kiuchumi.

“Niwaombe sana, maisha yanahitaji ubunifu, ujuzi na maadili, hivyo basi vyeti mlivyotunukiwa vikawasaidie kubadilisha maisha yenu na jamii. Pia kuweni na moyo wa kujaribu kwani ndio njia pekee ya kusonga mbele kimaisha.” Ameeleza Bw. Balandya.

Aidha, amebainisha kuwa serikali imekuwa ikiwashika mkono wananchi kwa kutoa mikopo kupitia mapato ya ndani ya halmashauri hivyo wahitimu na wananchi wanaalikwa kujiunga vikundi vya ujasiriamali na biashara zingine ili kuchukua mikopo hiyo ili waweze kujiinua kiuchumi na sio kusubiri kuajiriwa pekee.

Akiupongeza uongozi kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya chuo kwa kutumia mapato ya ndani hasa ujenzi wa bwalo la chakula litakalobeba watu 600 lililofikia 4% linalotarajiwa kugharimu Tshs. milioni 365 na hosteli itakayobeba wanafunzi 306 iliyofikia 70% huku likitazamiwa kugharimu bilioni 7.2 kwa kutumia mapato ya ndani Bw. Balandya amewasihi kuendelea kujitoa ili kufanya maendeleo yenye tija nchini.

Halikadhalika, amewataka wahitimu hao kuwa na moyo wa uthubutu, uadilifu, na utayari katika kubadilika kwa namna ambavyo dunia inaenda lakini pia kutumia teknolojia za kidigiti kama Akili Mnemba kwa ufasaha.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa chuo hicho Prof. William Pallangyo amewasihi wahitimu wote kutumia ujuzi na mafunzo waliyoyapata kuhakikisha wanaenda kuishi katika maisha halisi na kulijenga taifa.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.