Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Ngusa Samike amezitaka Halmashauri zote Mkoani humo kutenga viwanja vya kutosha kwa ajili ya kuendeleza soka la Wanawake.
Aidha, Samike amesema hayo wakati wa Kikao na baadhi ya Viongozi wa Soka la Wanawake kutoka Wilaya nne za Mkoa wa Mwanza ambapo amesema bado mazingira ya Soka la Wanawake hayaridhishi likiwemo suala la Viwanja.
"Nimejionea mwenyewe mazingira husika,viwanja vingi vimetawaliwa na soka la Wanaume,hivyo Wakurugenzi wote wa Halmashauri wataandikiwa barua kuhakikisha viwanja kwa Wanawake vinatengwa" amesema Katibu Tawala Ngusa Samike.
Akizungumzia hali ya Soka la Wanawake Mkoani Mwanza,Mwenyekiti wa Soka la Wanawake Mkoani humo,Sophia Makilagi amesema bado wanahitaji nguvu za Wadau kusukuma mbele mchezo huo.
"Ligi yetu bado hatujaanza kutokana na kukosa wadhamini japo tuna wachezaji wengi wenye vipaji" amesema Mwenyekiti Makilagi.
Mwamuzi mstaafu wa FIFA na muasisi wa Soka la Wanawake Mkoani Mwanza,Saada Tibamimale amesema kinachohitajika sasa ni mshikamano wa pamoja kati ya Wadau na Serikali ya Mkoa ili kuwa na timu endelevu za Soka la Wanawake.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.