RC MAKALLA AZIDI KUWAJAZIA MAPESA PAMBA JIJI FC SASA KILA GOLI ANUNUA KWA MILIONI MOJA
*Awapongeza matokeo ya mchezo wa ugenini dhidi ya Kengold*
*Awataka kukaza buti michezo minne iliyosalia*
*Awasihi kuepuka kurubuniwa na kusaliti timu*
Wakati filimbi ya kuhitimishwa michuano ya ligi ya Championship ikiwa ukingoni kupulizwa, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amezidi kuwapa ari wachezaji wa timu ya Pamba Jiji FC kwa kununua kila GOLI Sh. Milioni moja kwa michezo yao minne iliyosalia.
Makalla ambaye ni mlezi wa timu hiyo amesema hayo leo Machi 27, 2024 alipowatembelea wachezaji wa Pamba Jiji kwenye uwanja mkongwe wa Nyamagana, amesema mbali ya motisha hiyo pia amewapa Sh. Milioni 5.2 kama bonus yao kutokana na mwenendo mzuri na kucheza soka la kiwango hasa katika mpambano wa ugenini dhidi ya Kengold.
"Mimi sina maneno mengi zaidi ya kuwa mtu wa vitendo kama nilivyowaahidi,ule mchezo dhidi ya Kengold mliwafanya wenyeji wenu kama wapo ugenini kutokana na soka mliowatandazia na mwishowe tukatoka share ya 2-2 na kupata alama moja ambayo imetuweka pazuri", CPA Makalla.
Makalla ambaye ni mkereketwa wa soka ametaka Pamba Jiji FC kuwa na juhudi zaidi uwanjani kwa kufunga mabao mengi na hatakuwa na hiana kwenye kutoa fungu la pesa la magoli hayo na kuwasisitiza kutokubali kuruhusu mabao ya kufungwa.
"Hapa naomba tuelewane mkishinda 3-2 hapo natoa milioni moja tu kutokana na kuruhusu magoli mengi ya kufungwa,safu ya ulinzi na mabeki nataka kuona ukatili wa kutoruhusu mpinzani kuwapenya na kuwafunga," amehimiza Mkuu huyo wa Mkoa.
Katika mazungumzo hayo na wachezaji Makalla amewataka kutanguliza uzalendo na kutokubali kurubuniwa hasa kwa kipindi hiki cha michuano kuelekea ukingoni kutokana na timu zilizowakaribia kuweza kufanya fitna ili zipate nafasi.
Nahodha wa timu hiyo na mchezaji mkongwe Jerryson Tegete amemuhakikishia mlezi wao sasa wachezaji wote wsmeshaona njia nyeupe ya kucheza ligi kuu nsimu ujao,hivyo wataendelea kuzingatia maelekezo yote kuanzia kwake na dawati lao la ufundi.
Timu ya soka ya Pamba Jiji FC hadi sasa imejikusanyia kibindoni point 55 baada ya kucheza michezo 26 na kushika nafasi ya pili nyuma wa vinara wa kundi hilo Kengold wenye pointing 60 na Jumamosi watawaalika Polisi Tanzania mpambano utakaorindima kwenye uwanja wa Nyamagana.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.