RC MAKALLA AZITAKA HALMASHAURI KUWA NA MIPANGO INAYOJIBU KERO ZA WANANCHI MOJA KWA MOJA
*Asema ni lazima wananchi wasikilizwe na kutatuliwa shida zao*
*Ataka mipango ya kuongeza wigo wa Ukusanyaji wa Mapato*
*Aagiza udhiti wa Mapato kwa kusimamia mashine za kukusanyia mapato*
*Atangaza Mwezi Machi ni awamu ya usikilizaji kero Jimbo kwa Jimbo *
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza CPA Amos Makalla amezitaka Halmashauri kuwa na mipango madhubuti kwenye mpango wa Bajeti itakayojibu moja kwa moja shida za wananchi kupitia huduma zinazotolewa kwa jamii.
Ametoa wito huo mapema leo Februari 12, 2024 kwenye Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wakati akifungua kikao kazi kilichowakutanisha Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala, Wakurugenzi pamoja na Menejimenti za Halmashauri mahsusi kujadili maandalizi ya mipango na Bajeti kwa Mwaka 2024/25.
Pamoja na Maagizo sita ya kufuata katika uandaaji wa Bajeti, CPA Makalla amesema ni lazima viongozi na watendaji wadumu kwenye kusikiliza kero za wananchi na kuziwekea mikakati ya kuzitatua mara moja kwani wananchi wengi wamekua na shida mbalimbali za kimaisha wanahitaji kusaidiwa.
"Nimefurahi kwamba nimepata majibu yaliyofanyiwa kazi kutoka kwenye kila wilaya kupitia ziara yangu niliyoifanya kwenye kila Wilaya, na ndio maana wamekuja viongozi wakuu wa nchi lakini hakukua na mabango ya malalamiko hiyo ni faida ya usikilizaji wa kero zao na kuzitatua." CPA Makalla.
Aidha, Mhe. Mkuu wa Mkoa amefafanua kuwa katika kuhakikisha wananchi wanasikilizwa na kujibiwa vema kero zao ni vizuri wakapewa majibu kwa maandishi kwani inakua rahisi kwenye ufuatiliaji wa kero zao zilizobaki pamoja na kuweka kumbukumbu vizuri juu ya zoezi hilo.
Katibu Tawala Mkoa Balandya Elikana ametumia wasaa huo kuitaka Sekretarieti ya Mkoa na Menejimenti za Halmashauri na kuhakikisha katika upangaji wa Bajeti wanazingatia msingi unaoleta tija kwa wananchi wanaowatumikia pamoja na kuwa na vyanzo vipya vya mapato ili kupanua wigo wa ukusanyaji.
Aidha, amesisitiza kuzingatia mipango na mikakati ya udhibiti wa fedha za umma kwa kuzingatia matumizi sahihi ya mashine za mifumo pamoja na upelekaji wa fedha za mapato ya ndani kwenye miradi ya maendeleo kwa mujibu wa sheria pamoja na usimamizi dhahiri wa miradi pamoja na upelekaji wa fedha kwa makundi maalum.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.