Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Adam Malima amewataka viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kuweka mkazo kwenye zoezi la Sensa ya watu na Makazi linayotarajia kufanyika jumanne ya Agosti 23, 2022 nchini ili lifanikiwe kwa kiwango kilichokusudiwa.
Mhe. Malima amesema hayo Agosti 03, 2022 wakati akizungumza na Viongozi, watumishi na wadau wa maendeleo wilayani Nyamagana akiwa kwenye ziara ya kujitambulisha na kupata taarifa ya Maendeleo kufuatia kuteuliwa kwake kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza mwishoni mwa wiki.
Aidha, Mhe Malima amesema amefurahishwa na mwenendo wa Ukusanyaji wa mapato ya ndani kwenye Halmashauri hiyo na ametoa wito kwa Watumishi kuhakikisha wanaongeza wigo wa Ukusanyaji wa mapato na kuboresha upatikanaji wa huduma bora kwa jamii kama vofaa tiba kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya.
"Wananchi wa Nyamagana wamewakabidhi hatma ya maisha yao, nendeni mkaonekane kwenye Ukusanyaji wa Mapato, utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kupunguza hoja za mdhibiti na mkaguzi wa Hesabu za Serikali maana mimi nachukia sana kuwepo kwa hoja za kizembe kutokana na kutokujali." Mhe. Malima.
Aidha, ameagiza kupatiwa taarifa ya utekelezaji wa zoezi la mikopo ya asilimia kumi kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kutoka sehemu ya Ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri kwani ni kiu yake kuona usimamizi wa dhati kwenye eneo hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Makilagi amesema Ukusanyaji wa Mapato 2021/22 Halmashauri ya Jiji la Mwanza wamekusanya Zaidi ya Bilioni 18 sawa na Asilimia 103 ya makisio na wamekua wakitekeleza Miradi kadhaa ya kimkakati ukiwemo Mradi wa Stendi ya kisasa ya Nyegezi inayotekelezwa kwa Bilioni 23 ikiwa imefikia 76 ya utekelezaji.
Aidha, amesema Wilaya hiyo kupitia Halmashauri ya Jiji imekua ikitekeleza kwa dhati miradi mbalimbali ya Maendeleo katika sekta za Elimu, Afya, Uvuvi, Ufugaji na Miundombinu ambako kote wamekua mstari wa mbele kuimarisha jamii kwa kuwajengea uwezo katika shughuli wanazofanya.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.