RC MTANDA AAGIZA UCHUNGUZI KUBAINI CHANZO CHA MOTO KITUO CHA AFYA KAKOBE
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ametoa muda wa siku kumi na nne kwa Katibu Tawala Mkoa huo Bwana Elikana Balandya kuunda timu maalumu ya kuchunguza chanzo cha tukio la moto lililotokea usiku wa kuamkia September 02 katika kituo cha afya Kakobe kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa.
Mhe. Mtanda ametoa agizo hilo leo Septemba 02, mara baada ya kutembelea kituo hicho na kujionea madhara yaliyotokana na moto huo, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wananchi hao kuwa na subira katika kipindi hiki ambapo Serikali inaendelea kutafuta namna mbadala ya kuwapatia wananchi hao huduma muhimu ya matibabu.
Akiwatoa hofu wananchi zaidi ya elfu 20 wanaotumia kituo hicho, RC Mtanda amesema huduma zitaendelea kutolewa kama kawaida kwani Mganga Mkuu wa Mkoa atahakikisha anachukua hatua za dharula ili kuhamishia huduma za maabara kwenye jengo linalofaa.
Aidha, amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa kufanya tathmini kwenye uharibifu wa majengo hayo na kushauri kama yanastahili kukarabatiwa au vinginevyo ili hatua zichukuliwe mara moja za kuhakikisha huduma zinarejeshwa kwenye kata hiyo ya Kazunzu.
Akitoa taarifa ya tukio hilo la moto, Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo Dkt. Vita Ndohele amesema chanzo cha moto huo inasemekana ni hitilafu ya umeme katika chumba cha maabara na kupelekea kuungua kwa jengo la wagonjwa wa nje ambalo lina vyumba saba, kuteketea kwa vifaa tiba pamoja na dawa vilivyokua vikitumika ndani ya vyumba hivyo huku hasara ya dawa na vifaa tiba ikisemekana kuwa ni zaidi ya thamani ya shilingi Milioni 100.
Halikadhalika, amewashukuru wananchi kwa utulivu na ushirikiano katika kuokoa vitu visiteketee mara tu baada ya madhira hayo kutokea majira ya saa 7 usiku wa kuamkia leo kabla ya Taasisi ya uokoaji ya zimamoto kuwasili kwa msaada zaidi kutokana na umbali uliopo kutoka Mkoani.
Kituo hicho kilichoanzishwa tangu mwaka 1986 kimekua tegemeo kwa zaidi ya wananchi elfu 20 kutoka kwenye tarafa nzima ya Kakobe.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.