RC MTANDA AFUNGA MAFUNZO YA AWALI JESHI LA AKIBA 2024 SENGEREMA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda leo 17 Novemba, 2024 amefunga rasmi mafunzo ya awali ya askari wa jeshi la akiba Kimkoa 2024 yaliyofanyika katika shule ya Msingi Ngoma kata ya Igalula Wilayani Sengerema.
Akizungumza baada ya ukaguzi wa gwaride lililofana pamoja na maonesho mbalimbali Mhe. Mtanda amewapongeza wahitimu hao 111 waliohitimu kwa kulinda nidhamu, utii na subira wawapo kwenye mafunzo na hatimaye kuwa rasmi askari wa jeshi hilo kama kiapo chao kinavyowataka.
Aidha, amewataka kudumu kwenye kiapo cha kutetea uchumi wa nchi kwa kushiriki katika vitendo vya kupambana na maadui ujinga, maradhi na umasikini katika jamii wanayoishi kwa kuchapa kazi na kutoa hamasa kwa wananchi kuwa wazalendo na kujibidiisha katika masomo ili kujipatia maendeleo.
Vilevile, ametoa wito kwa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema kuhakikisha wanawapatia vijana hao mikopo ili wafanye shughuli za ujasiriamali na wawajengee uwezo hatimaye kuunda makundi yatakayokidhi sifa za utoaji wa mikopo kupitia makundi ya vijana, wanawake na wenye ulemavu.
"Katika uchaguzi wa Serikali za mitaa viongozi na wagombea wote nawasihi mkajiepushe na rushwa kwani ni adui wa haki na kiongozi anayepatikana kwa kutoa rushwa hatowahudumia wananchi kwa moyo wote bali atakua ni mtafuta maslahi." Amesema Mhe. Mtanda alopokuwa akizungumzia uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Naye Mshauri wa jeshi la akiba Sengerema Meja Erick Mateni mesema kuwa vijana hao wataimarisha ulinzi katika maeneo yao kutokana na ukakamavu na uzalendo waliopewa kama vile mbinu za kivita, usomaji wa ramani, ujasiriamali, uraia, usalama wa habari, madhara ya rushwa pamoja na kuzima moto.
Wakisoma risala wahitimu hao Lily Simon na Magreth Edward wametoa ombi la kupewa kipaumbele kwenye kazi za ulinzi hususani kwenye mgodi wa Sota Mining pamoja na kupatiwa mikopo kupitia kundi la vijana, wazee na wenye ulemavu katika Halmashauri.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.