Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ameipongeza Doris Mollel Foundation kwa kutoa shilingi bilioni 2 kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la Wodi ya Watoto Wachanga (Neonatal Care Unit) katika Wilaya ya Kwimba. Amesema kiwango cha ubora wa mradi huo ni cha juu na kinaleta matumaini mapya kwa huduma za afya mkoani humo.

Akizungumza Februari 19, 2026 wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi wa mradi huo Kwimba, Mhe. Mtanda amesema sasa watoto wachanga watapata matibabu sahihi na ya kisasa. Ameongeza kuwa pamoja na ubora wa jengo, huduma zitakazotolewa zitakuwa bora na imara, kwani tayari timu ya madaktari bingwa imeanza maandalizi ya utoaji huduma.

Amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026, Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba imepokea shilingi milioni 774.4 kwa ajili ya miundombinu ya sekta ya afya. Aidha, upatikanaji wa bidhaa za afya katika halmashauri umefikia asilimia 90, huku upatikanaji wa dawa mkoani Mwanza ukiwa asilimia 93 baada ya Serikali kuleta shilingi bilioni 1.2 kuboresha huduma hizo.

Mhe. Mtanda ametoa wito kwa wananchi kutunza na kuhifadhi miundombinu ya afya iliyojengwa ili iweze kudumu na kuendelea kutoa huduma bora kwa jamii. Amesisitiza kuwa uwekezaji huo una lengo la kupunguza vifo vya watoto wachanga na kuboresha viwango vya maisha.

Akisoma taarifa ya mradi, Msimamizi wa mradi huo, Mhandisi Alistides Leopord Kahigimo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba, amesema ujenzi unatekelezwa na Doris Mollel Foundation kwa ufadhili wa taasisi ya Keep a Child Alive ya nchini Marekani, iliyoanzishwa na msanii Alicia Keys.

Mradi huo unatekelezwa na mkandarasi Kiure Construction Company Limited na ulianza Mei 6, 2025, ukitarajiwa kukamilika ifikapo Februari 22, 2026. Hadi sasa umefikia asilimia 99.5, huku kazi zinazoendelea zikiwa ni usafi, ufungaji wa vifaa tiba, ukaguzi wa mifumo ya maji na umeme pamoja na umaliziaji wa nje.

Jengo hilo lina uwezo wa kuhudumia watoto wachanga 42 kwa wakati mmoja, wakiwemo watoto njiti na wenye changamoto mbalimbali za kiafya.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.