Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amesema nidhamu na kuwa na malengo ni msingi wa kuwa kiongozi mzuri na bora.
Mkuu wa Mkoa ameyasema hayo leo juni 30, 2025 wakati akimuapisha Mkuu wa Wilaya ya Magu Mteule Bi. Jubilate Win Lauwo, ambapo amesema kazi ya Kiongozi ni usimamizi na uratibu wa shughuli za Serikali katika ngazi ya Wilaya.
Mkuu wa Mkoa amesema kiongozi mzuri ni yule mwenye maono na mwenye kusimamia imani yake juu ya wale anaowaongoza, amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Magu atambue Wilaya yake inataka nini ameikuta wapi na lazima aweke malengo ya kuifikisha WIlaya hiyo mahali fulani.
“wewe una elimu kubwa, uzoefu wako wa miaka miwili katika Ukatibu Tawala na unajiamini kwa hiyo tunaanini utakwenda kufanya hii kazi kikamilifu”.
Kadhalika Mhe. Mtanda amesema ili uwe Kiongozi hodari lazima kuwa jasiri wa kuhakikisha unasimamia maono, maamuzi, na msimamo sahihi kuhusu ukweli maana ndio msingi bora wa uongozi.
“Ukishakubali kila unachoambiwa wewe unakuwa kiongozi ambaye unaendeshwa lazima uwe na msimamo, usiruhusu hilo”.
Kadhalika Mkuu wa Mkoa amemtaka Mkuu huyo wa Wilaya huyo kuweka maeneo ya kipaumbele ili mwisho wa siku akiondoka aache alama na kumtoa hofu kuwa hawezi kufanya kila kitu lakini lazima awe na eneo la kipaumbele inaweza kuwa upande wa elimu, mazingira, ulezi na masuala kama hayo.
Akizungumza mara baada kuapishwa Mkuu wa wilaya ya Magu Mhe. Jubilate Win Lauwo amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa nasaha zake za uongozi na kuahidi kufanya kazi kwa bidii kwa kile alichokisema kuwa kazi ni ibada.
Mkuu huyo wa Wilaya ya Magu ameapishwa leo kufuatia uteuzi wa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alioufanya terehe 23 Juni, 2025 na ameteuliwa kufuatia utenguzi wa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.