Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewataka wananchi wa Mwanza kuwa nguzo ya amani, maadili na mshikamano wakati wa Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya 2026.

Ametoa wito huo mapema leo Desemba 23, 2025 wakati akizungumza na wananchi, watumishi na viongozi katika hafla fupi ya kuwatakia wananchi kheri ya Sikukuu hizo za mwisho wa mwaka.

Mhe. Mtanda amesema mwaka 2025 umekua ni mwaka wa mafanikio kwani wananchi wamejielekeza kwenye shughuli za uzalishaji mali kwa amani na kupelekea kujiinua kiuchumi.

“Niwaombe Kamati ya Usalama tusiingie kwenye shughuli zao wakiwa wanafurahi na kuzima muziki, waacheni wananchi washerehekee sikukuu hizi kwa amani na utulivu wakiwa wanamshukuru Mungu wao kwa uhai.” Amesema Mhe. Mtanda

Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuwajibika kuilinda amani kwa kutoa taarifa pale watapoona kuna dalili za uvunjifu wa amani katika mitaa yao ili kila mmoja afurahie siku kuu za kuzaliwa kwa Kristo.

Sambamba na hayo, Mhe. Mtanda amewashukuru viongozi wa dini, watumishi, wananchi pamoja na wakuu wa taasisi kwa ushirikiano waliouonesha katika ofisi yake.

Vilevile, ametumia wasaa huo kumshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa kutoa zawadi za Krisimasi kwa vituo vya malezi ya watoto vilivyopo Wilayani Nyamagana na Ilemela na kwamba atakabidhi vyakula na vinywaji siku ya kesho.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.