Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewataka wakuu wa vyuo mkoani humo kutoa elimu kwa wanafunzi wapya wanaodahiliwa pamoja na kuweka usimamizi mzuri wa kuhakikisha wanajiunga na fao la matibabu kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

Mhe. Mtanda ametoa agizo hilo mapema leo jumatatu tarehe 10 Novemba, 2025 wakati akifungua kikao kazi kilichoitishwa na NHIF kwa wakuu vyuo 42 vya mkoani humo chenye lengo la kupitia hali ya utekelezaji wa usajiri wa wanafunzi kwenye mfuko huo kwa ajili ya kuleta utulivu wa kimatibabu kwenye vyuo vyao.

“Twendeni tukafanikishe kila mwanafunzi anakua ndani ya mfuko huu kwani tukikusanya kwa pamoja ndipo tutaweza kutoa huduma bora lakini tukikusanya kwa uchache mfuko utashindwa kujiendesha vema kwani wachache watasajiriwa na wakiugua wote kwa wakati mmoja italeta utegemezi.” Mhe. Mtanda.

Aidha, amebainisha kuwa jukumu la utekelezaji wa mfuko wa bima ya afya kwa wote ni la kila mmoja hivyo kila chuo kisimamie kwa makini adhma hiyo ili kujihakikishia wanafunzi na jamii kwa ujumla inakua na uhakika wa matibabu mara tu wanapougua.

Aidha, amewaagiza mfuko huo wahakikishe wanaboreaha mifumo ya usajiri pamoja na kushirikiana na serikali hususani Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kuondoa kwa haraka changamoto zinazochelewesha ukamilifu wa wanafunzi kwenye fao hilo.

Vilevile, ameviagiza vyuo kuwasilisha utekelezaji wa matakwa ya sheria ya bima ya afya kwa wote kwa kuhakikisha wawawasajili wanafunzi wote wanaostahili na kuwasilisha taarifa ya kila robo katika NHIF na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa ufuatiliaji.

Awali, Meneja wa Mfuko wa Bima ya Afya Mkoa wa Mwanza Ndugu Jarlath Nushashu alibainisha kuwa malengo ya kukutana na kundi hilo ni kupanga na namna ya kuimarisha na kuboresha usajiri wa wanafunzi wapya katika fao la wanafunzi ambalo lilianzishwa mwaka 2009 lililolenga kuwanufaisha wanafunzi kwa Tshs. 50,400 tu kwa mwaka.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.