Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ametoa wito kwa wananchi wote wenye umri wa kuanzia miaka 18 ambao wamekosa elimu ndani ya mfumo rasmi kutumia fursa ya uwepo wa vituo vya elimu ya watu wazima kupata maarifa na ujuzi.
Ametoa wito huo mapema leo tarehe 15 Septemba, 2025 akiwa katika uwanja wa Sabasaba Wilayani Magu kwenye kilele cha maadhimisho ya juma la Elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi Mkoa wa Mwanza.
Amesema, Mkoa huo una zaidi ya watu 2625000 ambao hawajui kusoma na kuandika na kwamba serikali imeanzisha vituo katika Halmashauri zote nane ambapo kuna zaidi ya wanafunzi elfu 36 wanaopatiwa elimu nje ya mfumo rasmi hivyo mi fursa ya kukimbilia kwa wote waliokosa.
Mhe. Mtanda amebainisha kuwa elimu ya watu wazima inajumuisha programu mbalimbali ikiwemo MEMKWA ambayo ni maalumu kwa ajili ya kuwawezesha waliokosa elimu ya msingi kupata stadi za kujua Kusoma, kuhesabu na kuandika ili kufuta ujinga.
Aidha, amebainisha kuwa ndani ya mfumo huo kipo kipengele cha MUKEJA ambacho kinatoa fursa ya kutoa maarifa kwa uwiano ambapo jamii inapewa stadi za ujuzi mbalimbali za ujasiriamali na akabainisha kuwa kuna zaidi ya wafungwa 300 mkoani humo wanapatiwa elimu hiyo.
Vilevile, ametumia wasaa huo kumshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fursa kwa vijana walioodolewa kwenye mfumo rasmi kwa sababu mbalimbali kama mimba, kupata tena nafasi ya kusoma na kutimiza malengo yao.
Akitoa taarifa ya Mkoa Dkt. Onesmo Nyamweru amesema juma jilo linaadhimishwa kila mwaka jirani na tarehe 8 septemba kwakua ndiyo siku ya Kisomo cha Kimataifa ulimwenguni kote na kwamba maadhimisho hayo yanatoa fursa ya kutafakari dhana na maendeleo ya Programu za elimu ya watu wazima kupitia maendeleo ya teknolojia.
“Elimu nje ya mfumo rasmi kitaifa imepanda kutoka 78% hadi 83% na kwa Mwanza wanaojua kusoma na kuandika ni 85.6% elimu hii ni nyenzo muhimu ya kupambana na umasikini, ujinga na maradhi na inakidhi mahitaji ya watu wazima ya sasa kwa jamii iliyo katika shughuli za uzalishaji mali.” Amesema Dkt. Nyamweru.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.