RC MTANDA AWAKABIDHI VYETI VIJANA WA HALAIKI KILELE CHA MWENGE WA UHURU 2024, AKEMEA UTORO SHULENI
Leo tarehe 13 Machi, 2024 Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewakabidhi vyeti vijana walioshiriki kwenye halaiki wakati wa kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru 2024 iliyofanyika kwenye uwanja wa CCM Kirumba tarehe 14 Oktoba, 2024.
Akiongea na vijana hao Mhe. Mtanda amewataka kuacha tabia ya utoro shuleni na badala yake wadumishe nidhamu na uzalendo ili kuendelea kuwa bora kitaaluma ili waweze kupata ufaulu mzuri utakaowasaidia kujitegemea katika maisha ya baadaye.
Aidha, amefafanua kuwa ndani ya muda huo mkoani Mwanza yamejengwa madarasa 306 ya shule za msingi, madarasa 2110 kwa Sekondari, matundu ya vyoo kwa msingi 1265 pamoja nyumba za walimu kwa msingi na Sekondari zaidi ya 80 zimejengwa pamoja na walimu 8465 wa msingi na Sekondari kupandishwa madaraja.
"Ndani ya miaka mitano ya uongozi wa Rais Samia mkoani Mwanza umejengea shule mpya 45, wanaodhani maendeleo nchini hakuna hawajatoka nje wakaona jinsi wenzetu wanavyoteseka lakini sisi tunasonga mbele tena kwa kasi." Mhe. Mtanda.
Amesema kuwa Serikali ya awamu ya Sita imejitanabaisha kuendelea kusimamia na kugharamia programu mbalimbali za elimu kuanzia ngazi ya awali hadi kidato cha sita kwani Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ana nia ya dhati ya kumpatia elimu bora kila mtanzania.
Aidha, ametumia wasaa huo kuwashukuru wazazi na walezi walioruhusu watoto wao kushiriki tukio hilo la kizalendo pamoja na wakufunzi wa kitaifa walioongozwa na ndugu Philipo Chogolela kwa kufanikisha halaiki mujarabu iliyoakisi nidhamu, ukakamavu na uzalendo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Ndugu Balandya Elikana amesema vijana zaidi ya 1350 walishiriki halaiki kwenye kilele cha mbio za mwenge wa uhuru 2024 kwa hamasa kubwa na kwa uzalendo ambapo walifundishwa kwa siku 60 na wakufunzi wa kitaifa na wa ndani.
"Mwanza hatuna jambo dogo, tulivunja rekodi kwa halaiki ya watoto hawa kwani ilifana sana na wageni na wenyeji walifurahia ukamamavu na ubunifu wa kutengeneza maumbo yaliyosawiri miradi ya kimkakati na waliimba wimbo wa kusifu Mkoa na walicheza ngoma ya kabila la wasukuma." Ndugu Elikana.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.