Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda leo Novemba 7, 2025 amewaongoza wafiwa,waombolezaji na watumishi katika mazishi ya aliyekuwa Baba mzazi wa Mkuu wa idara ya biashara, viwanda na uwekezaji katika Sekretarieti ya Mkoa Mzee Charles Karoli (92) katika makaburi ya familia Majengo - Ilula wilayani Magu.

Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw. Balandya Elikana ametoa salamu za pole kwa familia ya marehemu na amesema kwamba watumishi wote wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wanaungana na familia kwa kipindi hiki cha majonzi kwani wanajivunia upendo alionao Patrick kwa wenzake na ametoa rai kwa wana familia kumtegema mungu wakati wote hususani katika kipindi hiki kigumu.

Akiongoza ibada ya mazishi iliyofanyika katika kanisa Katoriki la Mt. Klaveri mjini Magu, Padri George Nzungu amewasihi waombolezaji kutengeneza mahusiano mema na Mwenyezi mungu kwa kufanya matendo mazuri ikiwa ni pamoja na kuwa na upendo baina yao huku akisisitiza kuwa upendo wa kweli huanzia katika familia zao hadi katika jamii.

Akimuelezea Marehemu, Padri Nzungu amesema marehemu Mzee Karoli aliishi maisha ya upendo na ukarimu kwa jamii iliyomzunguka na akahusianisha umati wa maelfu ya waombolezaji walioshiriki shughuli za mazishi hayo kuwa ni kutokana na mbegu ya kujali ambayo aliipanda mioyoni mwa watu enzi za uhai ambapo anatoa wito kwa jamii kumuenzi kwa matendo hayo mema.

Akitoa shukurani kwa niaba ya familia ya Mzee Karoli Mkuu wa idara ya biashara, viwanda na uwekezaji Bw. Patrick Karangwa amewashukuru waomboolezaji ikiwa ni pamoja na watumishi wenzake kwa kuonesha upendo wa kushiriki na kumsindikiza Baba yake mzazi katika safari yake ya milele.

Mzee Karoli alikua anasumbuliwa na maradhi ya saratani ya utumbo mkubwa na kwamba alipatiwa matibabu katika hospitali za BMC, KCMC,SHREE HINDU MANDAL, RABININSIA pamoja na Hospitali ya taifa Muhimbili ambapo umauti ulimfika Novemba 2, 2025.

Bwana ametoa, bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe. apumzike kwa amani. Amina.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.