Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ametoa rai kwa Wafanyabiashara Mkoani humo kuhakikisha wanachangamkia dawati la uwezeshaji biashara lililofunguliwa rasmi kwa kupeleka changamoto ambazo wanakumbana nazo ili waweze kunasuka na kuendelea kufanya biashara vizuri.
Mhe.Mtanda ameyasema hayo leo jumatano tarehe 03 septemba, 2025 wakati akizindua dawati maalumu la uwezeshaji biashara kwa maendeleo ya taifa kwenye viwanja vya TRA Mkoa wa Mwanza.
Mkuu wa Mkoa amesema dawati hilo ni muhimu sana na kutoa wito kwa Meneja wa TRA Mkoa wa Mwanza kuhakikisha dawati hilo linapatikana pia katika Wilaya zote za Mkoa wa Mwanza ili kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi kule waliko.
Aidha RC Mtanda ameeleza kuwa ukusanyaji kodi ni kitu muhimu katika kukuza uchumi wa Taifa na kuwataka Wafanyabiashara kutokukwepa kulipa kodi kwani Tanzania itajengwa na Watanzania wenyewe.
“Suala la kodi ni suala la nchi tunalazimika kulipa kodi, hatuwezi kuendesha serikali bila kulipa kodi hata maendeleo tunayoyaona leo katika Taifa letu kwa mfano juzi lile daraja la Kigongo -Busisi lililozinduliwa serikali ilitutangazia ni kodi zetu za ndani”.
Kila Mtanzania akilipa kodi kwa kiasi chake, kwa kiwango chake, mwenye kulipa elfu 20 alipe, anayetakiwa laki moja alipe anaye takiwa milioni moja alipe hapo ndipi tutaweza kulijenga Taifa letu. Ameongeza Mhe. Mtanda.
Awali,Meneja wa Mamlaka ya Mapato (TRA) Mkoa wa Mwanza Ndugu Faustine Mdesa amesema dhima ya kuwa na dawati hilo ni kutimiza maagizo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo amewataka TRA kuboresha mahusiano na wafanyabiashara kwa kuwasikiliza na kuwasaidia kutatua changamoto zao.
Akizungumza kwa niaba ya Wafanyabiashara, Jacob Paul amesema kufunguliwa kwa dawati hilo limewapa matumaini makubwa kwani wafanyabiashara wamekuwa na kero nyingi na sasa wamepata mahali pa kuziwasilisha ili zipatiwe ufumbuzi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.