RC MTANDA AWATAKA WATAALAMU SEKTA YA ARDHI KUWA WAADILIFU
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewakumbusha wataalam wa Sekta ya Ardhi Mkoa wa Mwanza kuepuka vishawishi vya rushwa, kufuata kanuni, taratibu na sheria za ardhi, na kuhakikisha kila kero au mgogoro wa ardhi unafanyiwa kazi na kufika mwisho ili kujenga imani kwa jamii na Wananchi kuhusu utendaji wa sekta ya ardhi.
Mhe. Mtanda ametoa kauli hiyo mapema leo alipokuwa akifungua kikao kazi cha wataalamu wa sekta hiyo Mkoani Mwanza, Mhe. Mtanda amesema kwa sasa wananchi wengi hawana imani ya utendajikazi na sekta hiyo hivyo wanapaswa kutenda haki na kufanya kazi kwa weledi wa juu.
Mkuu wa Mkoa amesema katika malalamiko ambayo huwa anasikiliza na kutatua kila siku ya Jumanne asilimia themanini ya malalamiko hayo ni ya sekta ya ardhi, hivyo amewataka kuona ukubwa wa tatizo na kulishughulikia ipaswavyo.
“Nimeongea hivyo ili muone ukubwa wa tatizo na changamoto hii imesababishwa kwa asilimia kubwa na wataalam wa ardhi wenyewe kwa kutotimiza majukumu yao”. Amesema Mhe. Mtanda.
Sambamba na hayo Mkuu wa Mkoa amesisitiza juu ya umuhimu wa kuandaa maandiko pamoja na kuzishirikisha taasisi na mashirika yasiyoya kiserikali, kuwashirikisha wananchi pamoja na kutumia teknolojia rahisi na za kisasa katika upangaji wa miji ili kuharakisha maendeleo yawananchi.
Aidha Mkuu wa Mkoa amemshukuru na kumpongeza kwa dhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassani kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kutoa kiasi cha Shilingi Bilioni 50, na kuipatia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ili zitumike kutekeleza mradi wa kupanga, kupima na kumilikisha maeneo nchini.
“Fedha hizo zilipelekwa kwenye Halmashauri 57 ikiwemo Halmashauri za Mkoa wa Mwanza ambazo ni Jiji la Mwanza (Milioni 800), Ilemela (Bilioni3.5) na Buchosa (Milioni 300), Sengerema (Milioni 200) na vyuo vitatu…”.
Naye Bi. Happyness Mtutwa Kamishna wa Ardhi Msaidizi wa Mkoa wa Mwanza amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kutoa elimu nzuri na ushauri uliolenga kuboresha na kuimarisha sekta ya ardhi Mkoani Mwanza na kuahidi kiwa yale yote aliyoyasema Mhe. Mkuu wa Mkoa yatatekelezwa kwa kiwango cha juu na kwa wakati.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.