Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda leo Februari 12, 2026 ameweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa Shule Mpya ya Msingi ya Amali iliyopo Kata ya Kishiri, Jijini Mwanza, huku akitoa maagizo kwa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kuhakikisha mradi huo unakamilika ndani ya muda wa wiki tatu kama ilivyopangwa.

Akizungumza baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo, Mhe. Mtanda amesisitiza umuhimu wa kukamilika kwa mradi huo kwa wakati ili kuwezesha wanafunzi kuanza masomo katika mazingira bora na rafiki kwa maendeleo yao ya kitaaluma na kijamii.

“Naiagiza Halmashauri kuhakikisha muda waliopewa wanautumia vyema. Shule hii inapaswa kuanza kufanya kazi rasmi mara tu baada ya kukamilika. Hatuna sababu ya kuchelewa,” amesisitiza RC Mtanda.

Katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa ametumia fursa hiyo pia kutoa pongezi za dhati kwa wazazi, walimu na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Igoma kwa kufanya vizuri katika matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2025, ambapo shule hiyo imeongoza kiwilaya katika Wilaya ya Nyamagana.

“Shule ya Sekondari Igoma imekuwa kinara wa ufaulu kwa Wilaya ya Nyamagana. Nawapongeza sana kwa matokeo mazuri. Endeleeni kuchapa kazi kwa bidii ili matokeo yawe bora zaidi mwaka hadi mwaka,” amesema.

Kwa upande wake, akisoma taarifa ya mradi kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Igoma, Anthony Masanja, amesema kuwa shule hiyo ilipokea kiasi cha Shilingi 330,700,000 mwezi Julai 1, 2025 kupitia Mradi wa BOOST kwa ajili ya ujenzi wa Shule Mpya ya Msingi ya Amali.

Ameeleza kuwa mradi huo unasimamiwa na Ofisi ya Mhandisi wa Jiji la Mwanza, huku mkandarasi anayetekeleza ujenzi huo akiwa ni Ndugu Eliawony Makundi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hadi sasa mradi umetekelezwa kwa asilimia 75, ambapo jumla ya Shilingi 258,600,000 tayari zimetumika. Kiasi kilichosalia ni Shilingi 72,100,000 kwa ajili ya kukamilisha kazi zilizobaki.


Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.