Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amezitaka Halmashauri za Mkoa huo kurejesha fedha za mapato ya ndani kwa wananchi kwa kuwajengea miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali kwenye vijiji.
Amesema sheria zinaelekeza kutumia asilimia 40 ya makusanyo ya ndani kutekeleza miradi katika sekta za afya, kilimo, uvuvi, afya, elimu na miundombinu ikiwa ni katika kurejesha fedha kwa wananchi kwani vyanzo vya makusanyo ya fedha hizo ni pamoja na ushuru utokanao na mazao.
Mhe. Mtanda ametoa kauli hiyo Wilayani Misungwi alipokua akikagua miradi ya maendeleo na kubaini kuwa halmashauri nyingi wanatekeleza miradi mingi kwa kutumia fedha kutoka serikali kuu zaidi ya zinazotokana na mapato ya ndani.
Aidha, amewapongeza halmashauri hiyo kwa kutumia kiasi cha Tshs. Milioni 50 kutoka kifungu cha mapato ya ndani ambazo zimejenga madarasa mawili katika shule ya sekondari ya Jitihada na kusaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani.
Kadhalika, ameiagiza Halmshauri ya Wilaya ya Misungwi kukamilisha Zahanati ya kijiji cha Nyamikoma (Tshs. 107 M), mradi wa upanuzi wa mtandao wa maji safi (Tshs.188 M) pamoja na barabara ya kiwango cha lami Majengo (Tshs.411 M) ili ianze kutoa huduma.
Mhe. Mkuu wa Mkoa amehitimisha ziara yake kwa kukagua ujenzi wa shule ya sekondari ya Mwasonge inayojengwa kwa zaidi ya Tshs. Milioni 715 na ameagiza mkandarasi kuweka madirisha ya vioo haraka ili kuzuia rangi kwenye madarasa kupata vumbi pamoja na vyoo ili wanafunzi wasipate magonjwa ya mlipuko.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.