Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ameziagiza Kamati za Ushauri wa kisheria Mkoa na Wilaya kuhakikisha wanasaidia wananchi kumaliza kero na changamoto zao na hatimaye kuondoa migogoro kwenye jamii.

Ametoa rai hiyo mapema leo tarehe 02 Disemba 2025 wakati akifungua kikao kazi cha viongozi wa Kamati ya Ushauri wa Kisheria Mkoa waliokutana na kamati za wilaya za mkoa huo katika ukumbi wa Bodi ya Pamba jijini Mwanza.

Mhe. Mtanda amesema ameanzisha na kuzindua Kamati ya Mkoa na za Wilaya ili kuona wananchi na wadau wengi wanapata elimu katika masuala mbalimbali ya kisheria na kutatua migogoro iliyopo kwenye jamii kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.

Aidha, ameipongeza Kamati ya Ushauri wa kisheria ya mkoa huo na kamati za wilaya kwa kuwa vinara wa kushauri wananchi, watumishi, taasisi na viongozi wa umma kuhusu masuala ya kisheria na akatoa wito makundi yote kuiona ili kupata ushauri na msaada kwa wakati.

Halikadhalika, ameziagiza ofisi za wakuu wa wilaya kuhakikisha wanashirikiana na kamati za ushauri wa kisheria kwenye maeneo yao kwa kuwa na kliniki maalumu za muda fulani ndani ya mwezi au juma za kusikiliza wananchi na kuhakikisha wanawatatulia kero zao mathalani za ardhi , mirathi na ndoa ambayo imekithiri.

Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri wa Kisheria Mkoa Wakili Mwandamizi Kabyemela Lushagara alibainisha malengo ya kikao kazi hicho kuwa ni kujengeana uwezo na kuandaa mpango kazi mfupi wa miezi sita na mrefu kwa miaka mitano wa utekelezaji wa shughuliza huduma za kisheria.

Aidha, amebainisha kuwa Kamati hiyo imejiandaa kuwahudumia wananchi kutoka kwenye maeneo yao bila kusafiri kwenda mjini kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya kutumia mtandao ambao watautambulisha siku za usoni.

“Wananchi wanapokuja kwetu kuleta changamoto wanapoteza muda, maono yetu ni kuweka mpango maalum wa kuwasikiliza na kuwatatulia kero kwa kutumia mtandao ili wasipoteze muda na kwa mpango wetu hadi kipindi cha miaka 2 tutakamilisha hilo.” Wakili Lushagara.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.