Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda, amefanya mazungumzo na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (Mb) ofisini kwake, yakilenga kuimarisha sekta za mifugo na uvuvi mkoani humo.

Mhe. Mtanda ameeleza changamoto ya upungufu wa chakula cha samaki licha ya kuongezeka kwa ufugaji wa samaki kwa vizimba, akiomba kuanzishwa kwa kiwanda cha chakula cha samaki.

Pia amebainisha fursa kubwa za uwekezaji katika eneo hilo, pamoja na umuhimu wa kuangalia upya shamba la mifugo la Mabuki ili kuvutia wawekezaji na kuongeza uzalishaji.


Ameongeza kuwa uboreshaji wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza kuwa wa kimataifa utarahisisha usafirishaji wa nyama na samaki ndani na nje ya nchi, huku akiomba wizara kusaidia kutatua changamoto za tozo nyingi kwa viwanda vya samaki.

Kwa upande wake, Waziri Kakurwa amesema wizara imepokea maoni hayo na itayafanyia kazi, akisisitiza kuwa ziara yake ya kikazi katika wilaya za Nyamagana, Ilemela, Sengerema na Ukerewe inalenga kusikiliza wadau na wananchi.

Ameahidi kushughulikia suala la Mabuki, kuimarisha usafirishaji pamoja na kuanzisha mamlaka na bodi ya kusimamia masuala ya mifugo.

Waziri pia amepongeza hatua zilizopigwa katika ufugaji wa samaki kwa vizimba na matumizi ya asilimia 10 ya mapato katika Wilaya ya Nyamagana akisisitiza kuongeza boti za doria na kuhimiza halmashauri zote zinazopakana na Ziwa Victoria kuhamasisha ufugaji wa samaki kwa njia hiyo.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.