Mhandisi Robert Gabriel, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza amewaagiza Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema kuhakikisha wanajenga Miundombinu ya Afya kwenye kila Kijiji ili kusogeza huduma za afya kwa wananchi.
Mhe Mkuu wa Mkoa ametoa agizo hilo mapema leo ijumaa baada ya kuibuka hoja ya 2019/20 ya Upungufu wa Miundombinu ya Sekta ya Afya kwa kukosa Zahanati kwenye Vijiji 16 wakati Baraza la Madiwani la Halamshauri hiyo lilipokutana kujadili Hoja za Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali.
Mhe Mkuu wa Mkoa ametoa rai kwa Halmashauri hiyo kutenga fedha kwa ajili ya Ujenzi wa Miundombinu ili kupunguza pengo lililopo na jamii ihamasishwe kuchangia maendeleo ya miradi ya afya ili kupata rasilimali zaidi.
"Naomba ubunifu uwepo ili tupate Zahanati kwenye kila kijiji, tukikubaliana kwenye kamati zetu tutafanikiwa na kule kijijini Mhe Diwani akitafuta mchanga na mawe kutoka kwa wananchi wake halafu Mkurugenzi akapeleka Saruji basi tutasogea hatutabaki hapa tulipo."
Aidha, ametoa rai kwa TAKUKURU kufuatilia utekelezaji wa miradi katika hatua za awali ili kuzuia upotevu wa fedha badala ya kusubiri mambo yaharibike na kupitia hilo amemuagiza Mkurugenzi kuhakikisha taratibu za kisheria zinafuatwa kwenye matumizi ya fedha.
"Lengo letu ni kuzuia hoja hivyo ni lazima tujifunze kufuata kanuni na taratibu za fedha na ninaona dalili zote za Halmashauri hii kuondokana na hoja zinazoepukika hivyo wataalamu naomba tushirikiane na waheshimiwa madiwani na kuwe na uwazi kwenye kila jambo." Mkuu wa Mkoa.
Vilevile, Katibu Tawala wa Mkoa Ngusa Samike amewaasa waheshimiwa Madiwani kutumia Hekima na busara katika kazi na kuongeza ushirikiano na wataalamu ambao wengi wao ni wageni kwenye Halmashauri hiyo ambapo amebainisha kuwa Halmashauri hiyo ipo kwenye marekebisho makubwa ya ufanisi ili kuwaletea maendeleo wananchi.
Kaimu Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali Mkoa wa Mwanza, Waziri Shabani amesema Mwaka 2020/21 Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema ilikaguliwa na kupata Hati yenye Shaka.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.