Leo Desemba 02, 2025 Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amefanya kikao na viongozi wa Kanisa la African Inland Church of Tanzania (AICT) katika Kanisa Kuu la Makongoro Jijini Mwanza, ambapo amewataka viongozi wa dini kuendelea kuhubiri amani, upendo na mshikamano katika jamii.

Katika mazungumzo hayo, Mkuu wa Mkoa amesisitiza kuwa Taasisi za Kidini zina nafasi kubwa katika kujenga na kudumisha umoja wa kitaifa, hivyo ni muhimu mahubiri na miongozo wanayotoa kwa waumini iwe ya kuimarisha uelewano na kudhibiti misuguano isiyo ya lazima.

Aidha, amewataka viongozi wa AICT Mkoani Mwanza kutokubali kutumika kugawa waumini wao, bali waendelee kuhimiza misingi ya umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi.

Amesema kuwa jukumu la Viongozi wa Dini ni kuhakikisha jamii inabaki kuwa na maadili, ustahimilivu na upendo bila kujali tofauti za kiimani, kikabila au kijamii.

Viongozi wa AICT wakiongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la AICT na Askofu wa AICT Dayosisi ya Mwanza Mussa Masanja Magwesela wamemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa ziara hiyo na kuahidi kuendelea kushirikiana na serikali katika kuhamasisha amani na maadili mema ndani ya jamii.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.