REDIO ZA JAMII ZATAKIWA KUELIMISHA UMMA KUFAHAMU MFUMO WA M-MAMA
Mganga Mkuu Mkoa wa Mwanza Dkt. Jesca Lebba ametoa wito kwa Redio za jamii kusaidia kuelimisha umma juu ya mfumo wa M-Mama unaotoa fursa ya usafiri wa dharula kwa Mama na Mtoto mchanga kuanzia kwenye ngazi ya jamii hadi kwenye vituo vya kutolea huduma wakati wa dharula.
Akifungua semina ya mafunzo kwa Redio za jamii kutoka mikoa ya kanda ya ziwa kwenye hoteli ya Gold Crest jijini Mwanza leo Novemba 08, 2024 Dkt. Lebba amesema wanahabari kutoka kwenye Redio za kijamii wana nafasi kubwa ya kusaidia wananchi kuweza kufahamu mfumo huo ulioletwa mahsusi kwa ajili ya kuokoa maisha.
Ameongeza kuwa katika tafiti zilizofanyika imeonekana kumekua na ucheleweshaji wa taarifa, miundombinu duni ya kufika kwenye vituo vya kutolea huduma pamoja na ucheleweshaji kwenye kupatiwa huduma mara wafikapo wagonjwa hospitali hivyo mfumo huo umekuja na suluhisho kwenye adha hizo.
"Ndugu washiriki, tangu kuanza kwa mfumo huu mpaka sasa zaidi ya dharula elfu 98 zimesafirishwa na kwa Mwanza pekee ni zaidi ya dharula elfu 6 kwa wastani wa 300 kwa mwezi zimefikiwa."
Amefafanua Dkt. Lebba.
Aidha, mganga huyo wa mkoa amezitaka halmashauri kuhakikisha magari ya wagonjwa (Ambulance) yanakua tayari kutoa huduma wakati wote pamoja na kulipa kwa wakati kwa madereva ngazi ya jamii kwa mujibu wa mkataba yaani ndani ya siku 14 tangu watoe huduma wawe amelipwa.
"Naamini redio zetu mtatusaidia sana kuelimisha jamii kuwa huduma hii inapatikana kuanzia ngazi ya jamii na kwenye vituo vya kutolea huduma, matumizi sahihi ya namba 115 kwa ajili ya kuwaokoa wajawazito pamoja na watoto wachanga." Amesema Mganga Mkuu.
Awali, Mratibu wa mfumo wa M-Mama kutoka Mkoa wa Mwanza Stanley Kajuna amesema kuwa walengwa waliokusudiwa zaidi ni mama mjamzito, mama aliyejigungua mpaja siku 42, mtoto mchanga hadi siku 28 na jamii kwa ujumla na kwamba tayari kuna madereva 4000 wamesajiriwa.
Katika kusaidia jamii, Mfumo wa M-Mama unachagizwa na kaulimbiu isemayo M- Mama Okoa maisha na inaendeshwa bila malipo yoyote kwa wateja kuanzia kwenye simu hadi usafiri wa kwenda kwenye kituo cha kupata huduma za afya.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.