Taasisi ya The Desk & Chair Foundation (TD&CF) imeahidi kujenga matundu matundu 12 ya vyoo kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure ili kukamilisha matundu 20 ya vyoo baada ya kukabidhi manane.
Matundu hayo manane ya vyoo ambayo yamegharimu zaidi ya sh. milioni 20.3 yamejengwa na Taasisi ya The Desk & Chair Foundation (TD&CF) Tawi la Tanzania kwa ufadhili wa Charty Walfare Aid ya Australia.
Akikabidhi vyoo hivyo kwa uongozi wa hospitali hiyo Mwenyekiti wa TD &CF, Alhaji Sibtain Meghjee alisema taasisi hiyo inafanya shughuli za kijamii kwenye sekta za maji, elimu na afya iliguswa na changamoto ya uhaba wa matundu ya vyoo inayoikabili hospitali hiyo ya rufaa ya Mkoa wa Mwanza,Sekou Toure baada ya kupokea maombi yakihusu tatizo la vyoo.
Alisema kuwa, wamejenga vyoo matundu nane ya vyoo kati ya 20 kwenye hospitali hiyo iliyojengwa miaka ya 70 ikiwa na matundu manne wakati huo kikiwa kituo cha afya na matundu hayo kwa sasa hayakidhi mahitaji kutokana na kuhudumia watu zaidi ya 600 kwa siku.
Alhaji Meghjee alisema kwa kutambua umuhimu wa afya bora kwa jamii inayohudumiwa hapo imejenga matundu manane ambapo matundu 12 yatajengwa wiki sita baadaye ili kukamilisha idadi ya matundu 20 ya vyoo yatakayohudumia watu 500 kwa siku, yawakiwemo ya watu wenye ulemavu, watumishi na wazee wa jinsia zote.
Alisema taasisi hiyo imedhamiria kuunga mkono juhudi za serikali za kuboresha afya za wananchi ili kuwaepusha na maradhi ya kuambukiza na kuwafanya kuwa na afya bora kuelekea uchumi wa kati wa viwanda, kwani bila afya njema ni vigumu mwananchi kushiriki shughuli za uzalishaji na maendeleo.
“Nina furaha kukabidhi matundu 8 ya vyoo ili vianze kutumika baada ya awamu ya kwanza ya ujenzi kukamilika vikiwa na vifaa vya usafi, tenki la maji la ujazo wa lita 5000,”alisema Alhaji Meghjee.
Mwenyekiti huyo wa TD & CF alisema ili vyoo hivyo vidumu aliuataka uongozi wa hospitali hiyo kusimamia kwa dhati ili miundombinu yake isiharibiwe kwa sababu yapo maeneo mengi waliyosaidia kujenga vyoo miundombinu yake imehabiriwa.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Sekou Toure Dkt. Bahati Msaki, akizungumza baada ya kupokea msaada huo wa vyoo, alisema hospitali hiyo inahudumia watu 500 hadi 700 kwa siku hivyo msaada huo umekuja muda muafaka kwa sababu namba ya wahitaji ni kubwa.
“Kwa niaba ya Bodi na uongozi wa hospitali tunashukuru sana The Desk & Chair kwa msada huu wa vyoo matundu 8 ambayo yamegharibu fedha nyingi.Bado taasisi hii inaendelea kujenga mengine 12 ili kukamilisha matundu 20, ili kukidhi mahitaji makubwa ya wagonjwa na wasindikizaji pamoja na watumishi”alisema Dkt. Bahati.
Hata hivyo, mbali na changamoto ya uhaba wa matundu ya vyoo kwa wagonjwa wa nje, pia wodi nyingi zina changamoto hiyo na kuomba watu wengine wenye kuguswa na hali hiyo kuiga mfano wa The Desk & Chair ili kusaidia kujenga miundombinu ya vyoo hospitalini hapo.
Dkt. Bahati alifafanua kuwa Hospitali ya Sekou Toure ambayo ilijengwa miaka 70 miundombinu yake ya vyoo matundu manne yalilenga kuhudumia watu 50 lakini kulingana na hadhi yake kwa sasa, inahudumia watu 700 kutoka nje kwa siku na hivyo kuwa na mahitaji makubwa ya matundu ya vyoo.
Wakati huo huo Uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure imemkabidhi cheti cha kutambua mchango wake Mwenyekiti wa Taasisi ya The Desk & Cair Foundation (TD &CF), Alhji Sibtain Meghjee.
Alhaji Meghjee alikabidhiwa cheti hicho na Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo Dkt. Bahati Msaki muda mfupi wa hafla ya kukabidhi matundu nane ya vyoo kwenye hospitali hiyo.
Akimkabidhi cheti hicho Dkt. Bahati alisema Alhaji Meghjee kupitia taasisi hiyo amefanya mambo mengi kwenye hospitali hiyo kwa kujenga jengo la kupumzikia pamoja na vyoo matundu saba kwa ajili wananchi wanaokuja kuona wagonjwa, lakini pia imejenga vyoo matundu manne kwenye jengo la kuhifadhia maiti.
“Tutakuwa ni wezi wa wafadhila tusipoenzi na kutambua mchango wa Alhaji Meghjee katika kusaidia jamii ikiwemo hospitali hii na wapokea huduma wake.Hivyo tunamkabidhi cheti hiki ikiwa ni kumbukumbu yake kwa mazuri aliyotufanyia hospitali ya Sekou Toure,”alisema Dkt.
Kwa upande wa alhaji Meghjee alishukuru kwa cheti hicho na kuahidi kitakuwa chachu ya kuendelea kusaidia jamii.
“Najisikia faraja kwa kupata zawadi hii ambayo itakuwa chachu ya kuendelea kusaidia jamii katika sekta mbalimbali kwa kushirikiana na serikali kuhakikisha wananchi wanatimiza ndoto zao,”alisema.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.