Leo, Januari 26, 2023 Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima ameweka Mawe ya Msingi kuashiria kuanza rasmi kwa Ujenzi wa Vivuko vipya vya Nyakaliko-Kome (Sengerema), Ijinga-Kahangala (Magu) na Bwiro-Bukondo (Ukerewe) vinavyojengwa na Kampuni Mzawa ya Songoro Marine Transport LTD kwa thamani ya zaidi ya Bilioni 17.
Akizungumza kwenye hafla hiyo iliyofanyika kwenye Karakana ya Mkandarasi kwenye eneo la Ilemela Mhe. Malima amebainisha kuwa kukamilika kwa vivuko hivyo kutasaidia kuboresha huduma za Usafiri kwa Wananchi hasa wanaoishi kwenye maeneo ya visiwa na itaboresha uchumi kwani utarahisisha upatikanaji wa mahitaji na shughuli za kila siku.
Aidha, amewapongeza kampuni ya Songoro Marine kwa kuaminiwa na Serikali na kupata Ukandarasi wa ujenzi wa Miradi mbalimbali ya Vivuko nchini ambapo akabainisha kuwa mpaka sasa kampuni hiyo inatekeleza Ujenzi wa vivuko 8 vyenye thamani ya zaidi ya Bilioni 33 ikijumuisha maeneo ya baharini kama Mafia-Nyamisati Mkoani Pwani.
Vilevile, amewataka kampuni ya Songoro Marine kukamilisha miradi hiyo kwa wakati na katika viwango vinavyokubalika ili viweze kuwahudumia wananchi kwa muda mrefu zaidi na viweze kuwa tiba kamili ya adha ya usafiri wa majini hasa wanaoishi kwenye visiwa vinavyozunguka Mkoa huo.
Ndugu, Ludovick Nduguye, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Ujenzi) amebainisha kuwa Wizara imewekeza zaidi ya Bilioni 50 kupitia TEMESA katika kuhakikisha wananchi wanaboreshewa Miundombinu ya usafiri na kwamba wamejipanga kupanua wigo wa bajeti kwa wakala huyo ili kuwahudumia zaidi wananchi.
"Mpaka sasa tumesaini Mikataba ya Ujenzi wa Vivuko Vipya vitano vyenye thamani ya Bilioni 36.5 na Bilioni 22 ya ukarabati wa Vivuko na pia Bilioni 4 kwa ajili ya kukarabati maeneo ya kuvukia na kufanya jumla ya Bilioni 60.3 katika kuhakikisha huduma za usafiri wa Majini zinaboreshwa." Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Umeme na Ufundi(TEMESA), Ndugu Lazaro Kilahala.
Vilevile, Kihangala amefafanua kuwa Kivuko cha Nyakalilo-Kome kitakua na uwezo wa kubeba abiria 800 na tani 170 yakiwemo magari madogo 22 na kile cha Bwiro-Bukondo kitabeba Abiria 200 na tani 100 ikiwa ni pamoja na magari madogo 10 na Ijinga- Kahangara Abiria 200 na tani 10 ikijumrisha magari madogo 10.
Mbunge wa Jimbo la Ukerewe Mhe. Josephat Mkundi ameishukuru Serikali kwa kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2020-25 kwa kuwatengenezea wananchi Vivuko na amebainisha kuwa Kivuko hicho kitawasaidia sana wananchi wa maeneo ya Bwiro hususani wanafunzi ambao wamekua wakitumia mitumbwi kwenda shule na kitachochea ufaulu kuongezeka.
"Namshkuru sana Mhe. Rais kwa niaba ya wananchi wa Buchosa kwa kuwajali, kivuko hiki ni kukubwa sana yaani watu 400 wamesimama na 400 wamekaa hapa tutaandika historia maana zamani tulikua na kivuko kidogo kinasukumwa hadi na upepo, naona sasa ndoto yetu inakwenda kutimia na kwakweli siku ya uzinduzi kule kwetu tutachinja ng'ombe 7 kwa furaha." Amesema Mhe. Erick Shigongo Mbunge wa Buchosa.
Naye, Mkurugenzi wa Kampuni ya Ukandarasi wanaojenga vivuko hivyo ya Songoro Marine Transport Limited, Meja Songoro amesema kampuni hiyo inatekeleza Ujenzi wa vivuko hivyo na miradi mingine yote wakizingatia viwango vya kimataifa na mpaka kufikia Julai 2023 watakamilisha Ujenzi kwa mujibu wa mkataba.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.