STORI YA BABA NA WATOTO WATATU WALIOKUMBWA NA UGONJWA WA KUTETEMEKA NA KUPOOZA MWILI YAMGUSA RC MTANDA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda leo Februari 12, 2025 amefika katika Mtaa wa Ibanda - Mkolani Wilayani Nyamagana kwenye familia ya Mzee Frednand Zephania yenye wanafamilia 4 wanaosumbuliwa na maradhi ya kutetemeka pamoja na kupooza mwili na kisha kuwapatia msaada.
Amesema alipata mfadhaiko sana baada ya kuona taarifa hiyo kwenye vyombo vya habari na akaagiza wasaidizi wake kufuatilia tatizo ni nini lakini pia mahitaji ya kuweza kuwasaidia familia hiyo na ndipo amefika kuona namna gani watapata matibabu.
Mhe. Mtanda mara baada ya kupata taarifa kamili kutoka kwa wasaidiizi wake ndio akaamua kutafuta namna ya kupata bima za afya kwa wagonjwa zitakazowasaidia kupapatiwa matibabu bila ya kulipa kiasi chochote.
“Bima hizi zina jumla ya gharama za shilingi milioni 2.1 ili kuwapunguzia mzigo wa gharama za matibabu ambapo mlikuwa mnalazimika kulipa fedha taslimu”. Amesema Mhe. Mtanda.
Sambamba na bima hizo, Mkuu wa Mkoa ameipatia familia hiyo mtaji wa biashara wa shilingi milioni tano (5) ili kusaidia mahitaji ya kila siku kama chakula na mahitaji mengine ya kila siku.
Katika hatua nyingine, Mhe Mtanda amemuagiza Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza kuwapatia familia hiyo kibanda cha kufanya biashara katika soko jipya la mjini kati ili mwanafamilia mmoja ambaye hajaathirika na changamoto hiyo aweze kufanya biashara na kumudu kuhudumia familia hiyo.
Aidha, Mkuu wa Mkoa ametoa wito kwa wadau mbalimbali watakaoguswa na changamoto iliyoikumba familia hiyo kusaidia kuongeza mtaji kwa wanafamilia hao ili waweze kupata mtaji mkubwa zaidi huku akimtaka Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt. Jesca Lebba kuwapa kipaumbele wakati wote watapohitaji huduma za dharula wapate usafiri mara moja.
Vilevile, Mkuu wa Mkoa ameitaka jamii kuwapa moyo na kuendelea kuisaidia familia hiyo ili waweze kupata faraja kwa changamoto wanayopitia.
Mke wa Mzee Zephania Bi. Bahati Makalle amebainisha kuwa katika nyakati tofauti Mumewe na watoto wake watatu wamepatwa na ugonjwa huo wa kutetemeka na kupooza mwili, aidha alifanya jitihada za kuwapeleka kwenye uchunguzi na kuonesha wana shida ya misuli.
Katika kumudu maisha binti wa mwisho aitwaye Basilisa Zephania alikua anafanya biashara lakini aliifunga kutokana na kuhitajika kumsaidia mama yake kuwauguza wanafamilia hao ambao ni Samson zephania, Judith zephania, Nathan Zephania pamoja baba yao mzee Zephania.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt. Jesca Lebba amesema waliunda timu ya wataalamu kuchunguza chanzo cha tatizo hilo ambalo kwa awali wamebaini matatizo ya misuli na kwamba wanaendelea kufuatilia ili kubaini chanzo hasa ni nini.
Sambamba na hilo Dkt. Lebba pia amewatoa hofu majirani wanaoishi kwenye mtaa huo kuchangamana na familia hiyo kwani uchunguzi wa kitaalamu unaonesha maradhi yanayowasumbua siyo ya kuambukiza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.