TRA MWANZA WAANDAA FUTARI MAALUMU KUWASHUKURU WALIPA KODI KWA HIARI
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Mwanza wameandaa futari maalumu kwa lengo la kuwapongeza Wananchi wa Mkoa wa Mwanza kwa kulipa kodi kwa hiari ambapo mpaka kufikia sasa tayari Mamlaka wamefikia lengo kwa kukusanya mapato kwa 104%.
Akizungumza katika futari hiyo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi amesema ulipaji wa kodi ndio msingi wa maendeleo ya Taifa, na kodi ndio uti wa mgongo wa miradi mbalimbali ambayo inatekelezwa na inayopangwa kutekelezwa na serikali.
Aidha, amewapongeza kwa kufikia lengo la makusanyo ya asilimia 104 na kuwataka kuendelea kutoa elimu ya ulipaji kodi kwa hiari, wananchi waelimishwe vizuri ili walipe kodi bila kushurutishwa na mtu yoyote kwa kuwa hayo ndio maelekezo na maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Mwanza Bw. Faustine Mdessa amesema walianza shughuli hiyo mapema jana ambapo walitoa msaada katika vituo viwili vya watoto yatima na leo wameamua kukutana na makundi mbalimbali ya wawakilishi wa wananchi kwa lengo la kuwashukuru na kurudisha shukrani kwa Wananchi.
“Niwaombe nyie ambao mmeshiriki sadaka hii maalumu muwe mabalozi wazuri wa ulipaji kodi mkawaambie wenzetu huko wawe wazalendo kwa kulipa kodi kwa hiari”.
Sheikh Wa Mkoa wa Mwanza Alhajj Hassan Kabeke naye amewapongeza Mamlaka hiyo kwa kufanya jambo jema la kuwakumbuka Yatima na wale wenye uhitaji, Aidha amesema katika mjumuiko huo kuna watu wa dini mbalimbali hiyo ikiwa ni ishara ya kwamba sisi Watanzania ni wamoja na hatuna budi kuendeleza mahusiano hayo mema.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.