Kutokana na ongezeko la watu na mahitaji ya ardhi kuwa makubwa katika maeneo mengi ya majiji nchini, Jiji la Mwanza limejipanga kufanya matumizi bora ya ardhi kwa kujenga madarasa kwa mfumo wa ghorofa ili kukidhi upatikanaji wa madarasa mengi katika eneo dogo.
Hayo yamebainika leo katika ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo aliyoifanya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda katika shule ya msingi ya mchepuo wa kiingereza na kukuta ujenzi wa madarasa 11 kwa mfumo wa ghorofa yanayogharimu zaidi ya Milioni 665 ambao umesaidia kupata madarasa mengi kwa eneo dogo.
Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Mhe. Mkuu wa Mkoa amewapongeza Jiji la Mwanza kwa ubunifu huo na kubainisha kuwa kwa kufanya hivyo wataweza kupata madarasa mengi kwenda juu na kufuta msongamano wa wanafunzi kwenye madarasa bila kuanzisha ujenzi wa shule mpya pembezoni.
Amesema, maendeleo ya teknolojia yanashabihiana na uamuzi huo kwani unaruhusu uwekaji wa mifumo yote muhimu katika miundombinu kwa gharama nafuu katika eneo dogo kwa kuwa na madarasa, maabara na matundu ya vyoo katika eneo moja.
Aidha, Mkuu wa Mkoa ameipongeza Sahule ya sekondari Nsumba kwa kufunga mfumo wa nishati asilia kwa ajili ya kupikia uliogharimu Tshs. Milioni 7.8 ambao amesema utasaidia kupunguza gharama za uendeshaji na kupunguza uchafuzi wa mazingira ukilinganisha na matumizi ya kuni ya siku za nyuma.
Pamoja na kuwapongeza kutokana na kufaulisha katika madaraja ya 1-3 kwa wanafunzi wote waliomaliza kidato cha sita 2025 shuleni hapo, Mhe. Mtanda amekagua ufugaji wa samaki kwa njia ya kisasa ya vizimba unaofanywa na vikundi vya vijana 4 katika Mwalo wa Luchelele waliokopeshwa Milioni 360 na halmashauri hiyo.
Sambamba na hayo Mkuu wa Mkoa ameshuhudia jinsi halmashauri ya jiji ilivyoamua kutenga Tshs. Milioni 150 kusaidia ujenzi wa kituo cha polisi cha Nyegezi kinachojengwa kwa Tshs. Milioni 232, Milioni 708 zilizojenga miundombinu ya Kituo cha Afya Mkolani pamoja na 300 zilizonunua vifaa tiba ili kuwasogezea huduma wananchi wa maeneo hayo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.