Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa 2025 Bw. Ismail Ali Ussi ameipongeza Balmashauri ya Wilaya ya Ukerewe kwa kuviwezesha kiuchumi vikundi vya vijana kwa kuwapatia mikopo kupitia mapato ya ndani katika fungu la asilimia 4 kwa mujibu wa sheria.
Ametoa pongezi hizo leo tarehe 24 Agosti, 2025 katika kijiji cha Namalebe wakati akikagua maendeleo ya mradi wa kikundi cha “Vijana Kazi Kwanza Furnitures Ukerewe” ambapo vijana 5 wamekopeshwa jumla ya Tshs. Milioni 25 na Halmashauri hiyo na kujikita katika shughuli za uchomeleaji vyuma na Samani.
Amesema, Ukerewe wametekeleza kwa vitendo juhudi za serikali ya awamu ya sita kwa kuwezesha makundi maalumu ya wanawake, wenye ulemavu na vijana ambao wanajumuisha asilimia 10 ya mapato ya ndani kwani vijana kupitia miradi kama hiyo wanajikwamua na suala la ajira.
Aidha, ametoa wito kwa Halmashauri hiyo kuendelea kuwafikia vijana na makundi mengine kupitia mikopo hiyo inayojumuisha asilimia 10 kwa kuwapa zabuni kwenye huduma na vifaa ili kuwasaidia kukuza mitaji kwa kupitia utoaji huduma na bidhaa.
Aidha, kiongozi huyo amekabidhi vifaa kwa makundi ya watu wenye ulemavu kwa ajili ya kuwawezesha kiuchumi na amewapongeza halmashauri kwa kuwanusuru waathirika 1807 wa ukatili na kuwapa msaada wa kisaikolojia na kuimarisha afya ya akili katika kituo cha Tunajitambua UTC Supplies.
“Twendeni tuhakikishe miradi yetu yote inalindwa ili iweze kutoa huduma kwa wananchi kwa muda mrefu” Amesema Bw. Ussi wakati wa uzinduzi wa Mradi wa upanuzi wa mtandao wa Maji katika kijiji cha Bugula uliotekelezwa kwa Tshs. Milioni 546.1 ambao unahudumia zaidi ya watu elfu 7.
Kabla ya kukagua miradi ya Barabara, Hoteli na Maduka, Mwenge wa uhuru umezindua huduma katika kituo cha afya Kigara kilichojengwa kwa zaidi ya Tshs. Milioni 700 kinachohudumia takribani watu elfu 50 kutoka katika vijiji vya Kituntu, Nduruma na Bukanda ambapo wananchi wametiwa shime kuiunga mkono serikali.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.