UKWEPAJI KULIPA KODI NI UKATILI UNALENGA KUUA UCHUMI WETU - RC MTANDA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ametoa rai kwa Viongozi wa Taasisi za Umma na zisizo za umma kuendelea kuwa mabalozi wazuri katika kulipa kodi na kuhimiza watumishi walio chini yao kidai risiti wakati wote wanapofanya manunuzi ya bidhaa au huduma ili tujenge uchumi wa nchi.
Mkuu wa Mkoa ametoa kauli hiyo usiku wa leo Februari 19, 2025, alipokuwa akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mlipa kodi iliyofanyika katika Ukumbi wa Rock City Mall, Ilemela na kuupongeza uongozi mzima wa TRA kwa kuja na wazo hilo la namna ya kipekee kabisa la kuwashukuru walipakodi.
Aidha, Mhe. Mtanda ametoa rai kwa kila mmoja kuhakikisha analipa kodi sahihi na kwa hiari kwani kodi hizi ndio zinarudi tena kwetu katika mfumo wa huduma mbalimbali ambazo serikali inazitoa kwa wananchi wake.
“Sambamba na hilo niwakumbushe Mamlaka ya Mapato Tanzania kuendelea kutoa elimu ya kodi kwa wananchi ili kila mmoja aweze kutekeleza wajibu wake jinsi inavyompasa”.
Sambamba na hayo Mhe. Mtanda amewapongeza walipakodi wote waliopongezwa kwa kulipa kodi zao vyema na amewasihi zawadi hizo walizopewa kuwa chachu kwao na kwa wengine wengi kujifunza ya kwamba kodi ni jambo la kizalendo na linahitaji ushirikiano wa pamoja kati ya serikali na wananchi wake ili kuiwezesha nchi kupiga hatua zaidi na zaidi.
Naye Bw. Faustine Mdessa, Meneja wa Mamlaka ya Mapato Mkoa wa Mwanza, amesema ujio wa wazo hilo inadhihirisha kwamba TRA inathamini mchango
wa walipakodi katika makusanyo ya mapato ambayo yanaiwezesha serikali kutekeleza mambo mbalimbali yakiwemo kuboresha huduma za afya, ulinzi na usalama wa nchi.
Kadhalika amesema kuna kuna baadhi ya wafanyabiashara wanakosa uaminifu na kuwarubuni wateja kwa kuwashushia bei za bidhaa na huduma ili kuwapa risiti za bei ambazo sio sahihi hali inayopelekea mapato mengi kupotea.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.