Waziri wa Afya, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu ameupongeza Mkoa wa Mwanza kwa kuongezeka kwa vituo vya afya vyenye nyota tatu kutoka kituo kimoja mwaka 2015 hadi vituo 116 mwaka huu na kupungua kwa vituo vyenye nyota ziro ambavyo vilikuwa 151 mwaka 2015 kufikia vituo saba mwaka huu.
Mwalimu amebainisha hayo alipokuwa akizindua Mpango mkubwa wa kuboresha Afya ya Uzazi kwa Wajawazito na Watoto (IMPACT) unaotekelezwa na Aga Khan Development Network kwa ufadhiri wa serikali ya Canada utakaogharimu shilingi Billioni 25 na kutekelezwa katika Halmashauri zote nane za wilaya 7 za mkoani Mwanza.
Mhe. Mwalimu alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha vituo vyote vya afya Tanzania vinanyota tatu ili viweze kutoa huduma bora ikiwemo huduma ya uzazi ya mama na mtoto
“Wanawake wengi hawapendi kujifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma kwa sababu ya lugha chafu na huduma mbovu, unapoona namba ya wanawake inaongezeka maana yake wana imani kubwa na huduma inayotolewa katika vituo vya mkoa ambao wameongezeka kutoka asilimia 67 hadi asilimia 77,”alisema Mwalimu.
Mhe.Ummy alifanya ziara katika kituo cha afya kwa huduma mashuleni katika Kata ya Nyamagana na kuangalia changamoto za kituo hicho na kuwashauri halmashauri ya Jiji la Mwanza kupitia mapato yake ya ndani kuweka mkakati wa kuanza ujenzi wa kituo hicho kisha wizara itaweka nguvu baada ya kuona hatua za awali.
Awali akimkaribishaMhe. Ummy kwenye jimbo lake, Mbunge Jimbo la Nyamagana Mhe Stanislaus Mabula alisema wilaya ya Nyamagana ina ongezeko kubwa la wakazi wa Nyamagana ikiwa idadi ya watu wafikao 460,000 wanawake 217,600, wanawake waliofikia uwezo wa kuzaa ni 186,600 huku wilaya ya Nyamagana ikikadiriwa kuwa na wajawazito wapatao huduma 15,666.
Aidha, Mhe Mabula amepongeza serikali kwa kuwezesha kupata 96%-98% ya fedha ya madawa na vifaa Tiba kutokea 46% iliyokuwa ukipata huko nyuma. Mhe Mbunge amemuomba Waziri kupitia wizara yake kuangalia namna ya ongezeko la wakazi pamoja na Wagonjwa wa dhalura Nyamagana na pamoja na hospital ya Mkoa wa Mwanza inavyoweza kupelekea kuwa na changamoto ya ufanisi kazini.
Akitoa neno la shukurani Naibu Meya wa Jiji la Mwanza Mhe Bhiku Kotecha amepongeza ufanisi mkubwa wa utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi wa CCM kwa vitendo katika Wizara ya Afya na kumshukuru waziri kuzidi kuitendea haki wizara hiyo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.