Kufuatia kuungua moto kwa bweni la wanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya Sekondari ya Wavulana Bwiru iliyopo wilayani Ilemela jana usiku wadau mbalimbali wametoa Misaada kwa wanafunzi walioathirika ili kusaidia kurejesha maisha ya wanafunzi hao katika hali ya kawaida.
Akikabidhi vifaa hivyo kwa wanafunzi, leo Juni 30, 2022 Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Mhandisi Robert Gabriel amewashukuru Mhe Mbunge wa Ilemela, Bwana Peter, Desk and Chair foundation, CRDB, Nyakato Steel, NMB na wadau wengine mbalimbali walioguswa na maisha ya wanafunzi hao.
"Kwa niaba ya uongozi wa Mkoa wa Mwanza na zaidi timu ya Maafa nipende kutoa shukrani za dhati kwa wadau mbalimbali walioguswa na kuwasaidia watoto wetu waliopata majanga na hapa tunaona watoto wamepata mabati, magodoro, vyombo vya chakula, suruali, mashati, viatu, Chandarua, Masweta na mashuka." Mkuu wa Mkoa.
Aidha, Mkuu wa Mkoa amewaondoa hofu wazazi na wananchi kuwa watoto kwenye shule hiyo wapo salama na masomo yanaendelea kama kawaida kwani huduma zote zinaendelea kutolewa na wanafunzi hao wameshaanza kupata vifaa.
"Sisi kama wilaya ya Ilemela, tunakushukuru sana Mhe Mkuu wa Mkoa kwani usiku wa jana ulituahidi kuwa ndani ya saa 24 vifaa vilivyoteketea vitapatikana na kwa maelekezo uliyoyatoa tunakuahidi tutatumia siku tatu tu tunakamilisha ujenzi wa jengo la bweni lililo pale juu." Mhe. Salumu Kalli, Kaimu Mkuu wa wilaya ya Ilemela.
"Kwa niaba ya Benki ya NMB tunawapa pole wanafunzi wote kwa janga lililowapata, tuliposikia janga hili limetokea tumeamua kuja kuwapa pole na tumeambiwa kuwa kuna bweni linajengwa na lipo kiwango cha kuezeka nasi tumekuja na bati bando 11 zenye thamani ya Tshs Milioni 5." Meneja wa Kanda wa NMB, Baraka Ladslaus.
"Tatizo au janga hili lisiwavunje moyo, muwe na ujasiri na endeleeni kuwaombea waliowafadhili tena fanyeni jitihada kwenye masomo kwani kupata nafasi kwenye shule hii si kazi nyepesi hivyo nyie mna bahati sana. Amesema Alhadj Sibtain Meghjee, Mwenyekiti Mkaazi wa Desk and Chair foundation aliyetoa Msaada wa Magodoro, Vyandarua na shuka vilivyogharimu Tshs Milioni 3.4
Awali, Mkuu wa Shule hiyo Mwalimu Thomas Werema alisema moto umeteketeza vifaa vyote vilivyokuwemo kwenye bweni la wanafunzi majira ya saa 3 usiku wakati wanafunzi wakiwa darasani wanajisomea na waliopata majanga ni wanafunzi 76 lakini wote wapo salama hakuna aliyedhurika.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.