Mganga Mkuu Mkoa wa Mwanza Dkt. Jesca Lebba amewaasa wahitimu wa kutoka sekta ya afya kutumia elimu waliyoipata kuitumikia jamii si tu kwa utabibu bali kwa kuleta fikra chanya zenye kuleta mabadiliko ya kifikra na kuweza kulinda afya zao.

Dkt. Lebba amesema hayo kwenye mahafali ya kumi na mbili ya chuo cha afya Tandabui yaliyofanyika Desemba 21, 2025 wakati akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.

Amesema taifa linahitaji wataalamu wa kutosha haswa katika fani za afya ambao watashughulika na afya za wazalishaji ambao watalisaidia taifa kufikia uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda.

“Ili Tanzania iweze kuwa nchi ya uchumi wa kati inayoongozwa na viwanda ni lazima kuwa na wataalamu wa kutosha katika fani za Afya ambazo zitashughulika na kuimarisha Afya za wazalishaji katika uchumi wa kati Wataalamu hawa hupatikana pale inapotolewa elimu iliyo bora na walimu walio makini”. Amesema Dkt. Lebba.

Aidha, amesema serikali imejipanga kuendelea kuimarisha na kuboresha sekta ya afya na kuleta maendeleo endelevu hususani kwa Mkoa wa Mwanza ambapo jumla ya Shilingi Bilioni 63.2 zimetolea kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya afya.

“Kuna miradi mikubwa ya serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyofanyika katika kipindi cha awamu ya sita hapa mkoani Mwanza ambapo jumla ya Shilingi Bilioni 63.2 zimetolewa katika Sekta ya Afya kwa ajili ya kuboresha miundombinu na ununuzi wa dawa na vifaa tiba”. Amesema Dkt. Lebba.

Sambamba na hayo ameupongeza uongozi wa wa chuo cha afya Tandabui kwa kutoa elimu bora na kuzalisha wataalamu kupitia ufundishaji unaozingatia mitaala ya ya afya inayoendana na uhitaji wa soko la ajira.

“Nawapongeza Tandabui kwa juhudi zenu za kubuni na kuboresha ufundishaji wenu kwa kuzingatia mitaala ya afya ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira na kukabiliana na uhaba wa wataalamu nchini katika fani za afya”. Ameongeza Dkt. Lebba.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.