Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Bwana Ismail Ali Ussi amewaasa wananchi kushiriki Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025 kuwachagua Wabunge, Madiwani na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ametoa wito huo leo Agosti 31, 2025 wakati akiongea na wananchi katika kijiji cha Bukokwa na maeneo ya jirani wakati akikagua utekelezaji wa ujenzi wa maduka 20 yanayojengwa kwa fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo kwa lengo la kupata chanzo cha kudumu cha ukusanyaji mapato.
Bwana Ussi amewasisitiza wananchi hao kuhusu umuhimu wa kujitokeza kupiga kura na kuzingatia taratibu za kisheria siku ya uchaguzi ili kulinda amani ya nchi.
Kadhalika amewataka vijana kutokutumiwa na wanasiasa wenye malengo ya kujinufaisha binafsi kwa kuanzisha vurugu, na badala yake amewataka kuwa mabalozi wa amani na mshikamano katika kipindi chote cha uchaguzi.
Aidha, amewasihi katika kuamua ni nani wa kumchagua wahakikishe wanachagua viongozi sahihi ambao wana kiu ya kuwaletea maendeleo kupitia atakayewapigiania kuwaletea huduma bora za kijamii kama maji safi na salama, elimu na pembejeo za kilimo.
Kadhalika, amewaalika kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi huo ili kuleta maana ya Uchaguzi mkuu ukilinganisha na idadi ya wananchi waliojiandikisha na kuboresha taarifa zao katika daftari la kudumu la wapiga kura katika zoezi lililoendeshwa na Tume huru ya Uchaguzi.
Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa ni Halmashauri ya nane (08) na ya mwisho kwa Mkoa wa Mwanza kukimbiza Mwenge wa Uhuru mwaka 2025 chini ya kaulimbiu isemayo ‘Jitokeze kushiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa Amani na Utulivu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.