“Wananchi wanapaswa kubadili mtindo wa maisha na kuzingatia lishe bora ili kuepuka magonjwa ya moyo,” amesema Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani yaliyofanyika leo Septemba 29, 2025 katika Uwanja wa Hospitali ya Kanda ya Rufaa ya Bugando, Jijini Mwanza.
Maadhimisho hayo yamelenga kuongeza uelewa kuhusu magonjwa ya moyo, ambayo yamekuwa chanzo kikuu cha vifo duniani, na yamehudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka sekta ya afya, mashirika yasiyo ya kiserikali na wananchi wa kawaida.
Akizungumza mbele ya mamia ya wananchi waliohudhuria, Mkuu huyo wa Mkoa amesisitiza kuwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza, ikiwemo maradhi ya moyo, yameendelea kuwa chanzo kikuu cha vifo nchini na duniani kote, hali inayohitaji hatua za haraka.
Kadhalika, Mkuu wa Mkoa amewataka wananchi kujenga tabia ya kupima afya mara kwa mara na kutambua hali ya moyo wao mapema kabla ya kuathirika zaidi.
“Tusiishi kwa mazoea ya kwenda hospitali tu pale tunapougua. Magonjwa ya moyo yanaweza kuzuilika iwapo tutajenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara na kuchukua hatua mapema,” amesema RC Mtanda.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando (BMC) Sr. Dr. Alicia Massenga amesema 20% ya watoto wanaozaliwa katika Hospitali hiyo wanakuwa na changamoto ya moyo na nusu yao wanahitaji matibabu ya upasuaji hivyo kulazimika kupelekwa JKC.
Amesisitiza kuwa bado suala la uelewa liko chini na kupelekea kuleta wagonjwa wakiwa wamechelewa hivyo kupendekeza uwepo wa utoaji wa mafunzo endelevu na upimaji wa moyo katika vituo vya afya.
Naye, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt. Jesca Lebba amesema Mwanza kuna jumla ya vituo 565 vinavyotoa huduma ya afya ikiwemo Bugando na elimu mbalimbali kuhusu masuala ya Afya imekuwa ikitolewa ikiwemo Moyo, lishe, umuhimu wa mazoezi.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Kila Pigo la Moyo ni Maisha, Lilinde Usilipoteze”.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.