WAZIRI MKUU AWATAKA WANAMALYA KUCHANGAMKIA FURSA YA CHUO CHA MICHEZO
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.) amewataka Wananchi wa eneo la Malya Wilayani Kwimba kujipanga kuboresha na kufanya maendeleo kwa kuwa uwepo wa Chuo cha Michezo katika eneo hilo ni fursa muhimu ya kiuchumi.
Waziri Mkuu ametoa rai hiyo leo mei 18, 2025 alipokuwa katika ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa Chuo cha Michezo Malya (Sports Academy) ambapo amewataka wananchi kuhakikisha wanajenga miundombinu bora ya malazi na makazi kwa kuwa siku za usoni mji huo unakwenda kubadilika.
“Zaidi ya biliono 32 zitaletwa hapa kuubadili mji huu wa Malya, jipangeni vizuri huu mji unakwenda kubadilika”. Amesisitiza Waziri Mkuu.
Kutakuwa na wageni, wachezaji wa mpira kutoka maeneo mbalimbali watalala wapi? wataishi wapi? watakula wapi?, mna kila sababu ya kujipanga kweli kweli na hii ndio Malya anayoitaka Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ameongeza Mhe. Waziri Mkuu.
Sambamba na hayo Mhe. Waziri Mkuu amepongeza kasi ya mradi hio na ubora wa majengo, na amesema kuwa ameridhishwa kusikia kuwa hakuna deni fedha zinazotakiwa kuletwa zimeletwa kwa wakati.
Katika Taarifa ya Mradi iliyosomwa na Bw. Gerson Msigwa Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imesema mradi huo ni moja ya miradi ya mkakati ya Serikali ya awamu ya sita ya kuhakikisha inaendeleza selta ya michezo katika Mkoa wa Mwanza na maeneo mengine nchini.
Kwa upande wake Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Mhe. Professa Palamagamba Kabudi amesema Mradi huo utatekelezwa katika awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza itachukua muda wa miezi kumi na mbili (12) na awamu ya pili ni muda wa miezi sita.
Aidha amesema jumla ya kiasi cha shilingi 31,523,920,683.60 kimetengwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Habari Sanaa Utamaduni na Michezo kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo ambazo zimepangwa kulipwa katika awamu mbili(2).
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.