BARABARA YA USAGARA - MWANZA MJINI KM 25 KUJENGWA KWA NJIA NNE
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi inachukua hatua za haraka kushughulikia msongamano wa magari kwenye Barabara Kuu kutoka Mwanza Mjini hadi Usagara kwa kuijenga kwa njia nne.
Ulega amesema hayo mkoani Mwanza wakati akizungumza na wananchi wa Buhongwa na kuongeza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amempa maelekezo ya kutafuta mkandarasi kwa ajili ya ujenzi huo ambapo Barabara mbili zitatoka Mwanza Mjini kuelekea Usagara na nyingine mbili kutoka Usagara kwenda Mwanza Mjini.
“Tumepanga kuhakikisha kuwa mchakato wa kumpata mkandarasi unakamilika ifikapo katikati ya Februari mwaka huu na baada ya kumpata mkandarasi, tutakuwa hapa Buhongwa kumkabidhi rasmi eneo la mradi ili aanze kazi mara moja ya ujenzi wa hizi kilomita 25 za barabara hii”, amesema Waziri Ulega.
Aidha, ameeleza kuwa katikati ya Barabara hizo kutakuwa na eneo la wazi kwa ajili ya mipango ya baadaye na kuongeza kuwa Taa za Barabarani zitawekwa kwa wingi ili kuboresha usalama hasa kutokana na shughuli nyingi za biashara zinazofanyika usiku na mchana katika eneo hilo.
Katika hatua nyingine Waziri Ulega ameagiza hifadhi za Barabara zinazotumiwa na wafanyabiashara wadogo zijengwe kwa ubunifu, huku akiwasihi viongozi wa Wilaya kushirikiana na wawekezaji kuhakikisha maeneo hayo yanaboreshwa kwa gharama nafuu.
“Rais Samia amekuwa mstari wa mbele kubuni njia za kuwasaidia wananchi kufanya biashara kwa ufanisi ni jukumu letu kuhakikisha tunatengeneza mazingira mazuri ya kiuchumi kwa kila mtanzania kupata riziki yake,” aliongeza.
Ujenzi wa Barabara nne, uwekaji wa Taa za Barabarani, na kubuni njia za usalama kwa wananchi si tu kutapunguza msongamano na ajali, bali pia kutaimarisha uchumi wa eneo hilo na maisha ya watu kwa ujumla.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.